Thursday, 1 June 2023

Mtambue mdudu msumbufu katika nyanya (kamtangaze)

Kantangaze ni Mdudu anayejulikana kama nondo wa nyanya, na kitaalamu Tuta absoluta, aligundulika kuwepo nchini tangu mwaka 2014, na anaathiri uzalishaji wa nyanya kwa kasi na kiasi kikubwa sana jambo lililopelekea wakulima kumpatia jina la “kanitangaze”. Ni muhimu kwa wakulima kumtofautisha mdudu huyu na yule mwenye mapindo, ambae kwa kawaida hushambulia nyanya na mazao mengine. Wadudu wenye mapindo ni aina ya inzi-buu lake huzalisha kijumba chembamba, ambacho husukwa kwenye majani, lakini hakishambulii tunda kama ilivyo kwa Tuta absoluta. Tuta absoluta ni nondo na buu lake huzalisha vijumba vikubwa, ambavyo hushambulia tunda la nyanya na hatimae kusababisha hasara kubwa kwa mkulima.

Tabia za wadudu hawa
Wadudu wakubwa wanafanya kazi usiku na mapema wakati wa asubuhi. Majira ya saa 1 hadi 5 asubuhi wanaweza kuonekana wakiruka kwenye sehemu ya juu ya mmea. Muda unaobaki wa siku wanajificha kwenye sehemu ya chini ya majani. Kwa kawaida huwa wanataga mayai usiku kwenye sehemu ya juu ya mimea, kwenye sehemu ya chini ya majani au shina changa au sehemu za maua. Katika maisha yao, mdudu jike huweza kutaga hadi mayai 260. Mayai yanapoanguliwa, mabuu hutumia masaa machache kujilisha juu ya mmea. Baada ya hapo, wanaingia ndani ya mmea ambapo hukaa hadi wapevuke na kuwa wadudu wakubwa. Baadhi ya mabuu walio kwenye mabadiliko huondoka kwenye pango walilopo na kuanzisha jingine, wakati mwingine ni ndani ya tunda. Buu mmoja linaweza kuharibu tunda zima kwenye shada. Wakati mabuu wanapozunguka mmea, wanafanya haraka sana kwa msaada wa nyuzi nyororo walizotengeneza.

Ukuaji
Ukuaji wa buu hufanyika kwenye udongo na kwenye mimea yenyewe. Mdudu anapopevukia kwenye mmea, hutengeneza kijumba chenye nyuzi laini ili kujilinda. Tuta absoluta ana uwezo wa kuwa na vizazi vingi katika kipindi cha miezi 12. Katika maeneo yenye joto, mzunguko unaweza kukamilika chini ya mwezi mmoja. Kutokana na muda wa mzunguko wa maisha kuwa mfupi, kuna hatua nyingi za mdudu huyu kuharibu mmea kwa kila kipindi kimoja cha maisha yake. Wadudu hawa hawapendi baridi kali wala joto kali sana. Chini ya nyuzi joto 10 inazuia ukuaji wa mdudu huyu, na zaidi ya nyuzi joto 30 hufa.

Uharibifu
Wadudu hawa husababisha uharibifu enezi wa jani pamoja na tunda, ambao unaweza kusababisha hasara ya asilimia 100 kwa mkulima. Mimea ya nyanya inashambuliwa kuanzia hatua za awali, hadi inapotoa matunda. Uharibifu wa awali hupelekea hatua ya pili ya maambukizi ya kuvu na bakteria. Buu linaweza kushambulia tunda mara tu linapotengenezwa. Huharibu pia vichipukizi ambavyo husababisha ukuaji mbovu wa mmea.

Udhibiti
Kwa kawaida utunzaji wote wa mazao hutegemea maamuzi madhubuti na utunzaji sahihi wa shamba. Kwa upande wa utunzaji wa mazao, mdudu mharibifu anatakiwa asipate chakula kwenye mmea unaomhifadhi.

Ili kudhibiti wadudu hawa,
zingatia mambo muhimu yafuatayo:
• Usipande tena mazao hifadhi mara tu baada ya uzalishaji wa mazao hifadhi ya mwanzo.

• Rudia kupanda mazao yasiyokuwa jamii ya mnavu

• Unaweza kuacha eneo hilo kwa muda wa wiki 5 hadi 6 bila kuwa na mimea hifadhi. Hali hiyo itasaidia kuondoa kizazi cha wadudu hao katika eneo hilo

• Ondoa magugu yote yenye majani mapana. Weka mkazo kwenye kuondoa magugu jamii ya mnavu

• Ondoa mara moja masalia ya mazao ya zamani, kisha yafukie

• Ondoa nyanya zilizoharibiwa kutoka kwenye mmea na uziteketeze

• Kuwa makini na utendaji wa majirani katika mashamba yao

• Pangilia eneo lako vizuri kwa kuweka nafasi kutoka katika shamba la jirani

Shughuli za binadamu
Mdudu huyu anasambaa kwa haraka sana kutokana na shughuli za binadamu. Ni muhimu kufanya juhudi ili kuzuia uenezaji unaotokana na shughuli hizo.

Tuta absoluta wanaweza kutaga mayai kwenye miche iliyopo kwenye kitalu. Hivyo kabla ya kutoa miche kwenye kitalu ni lazima ichunguzwe kwa umakini, ili kuona kama kuna dalili za wadudu waharibifu.

Endapo wafanyakazi wamekuwa kwenye shamba lililozagaa wadudu, ni muhimu kuhakikisha kuwa hawabebi wadudu kwenye nguo zao kutoka eneo moja kwenda lingine.

Hakikisha kuwa hakuna tunda lililoathiriwa na mdudu linalopelekwa sokoni. Tunda lililoharibika liteketezwe.

Vikapu na matenga yanayotumika kuvunia kwenye eneo lililoathirika, visipelekwe kwenye eneo safi ambalo halijaathiriwa.

Viuatilifu
Kuna aina nyingi za viuatilifu vinavyoweza kuua aina hii ya wadudu- “Tuta absoluta” lakini kuna mambo mengi yanayowasaidia wasife kwa urahisi.
• “Kanitangaze” Tuta absoluta, hujificha wakati wote. Anapokuwa mkomavu hujificha chini ya majani au mabuu ndani ya majani au tunda. Hali hii hufanya viuatilifu vya mguso au kunyunyiziwa kushindwa kuleta mafanikio.

• Mdudu huyu hujenga uwezo wa kushindana na dawa zilizotumiwa kupita kipimo.

Http//www.kilimoniuhaiblog.blogspot.com

Read less
image

0 comments: