KILIMO CHA MIGOMBA : Ndizi zapatikana kwa aina nyingi na wataalamu huhesabu takribani aina mia moja,100. Kwa matumizi ya kibinadamu aina zifuatazo zatofautishwa kufuatana na matumizi: kuna mtwike, za kilosa na Morogoro, kiwila nk.
Ndizi tunda la moja ya mimea ya jenasi ambayo huitwa migomba. Asili yake ni maeneo ya Kusini mwa Asia, na inawezekana kwa mara ya kwanza ilikuzwa huko Papua New Guinea. Leo, ndizi hulimwa maeneo mengi ya tropiki.
Ndizi zipo katika familia ya Musaceae. Hulimwa hasa kwaajili ya matunda yake, na mara kadhaa kwaajili ya uzalishaji wa nyuzi na kama mimea ya mapambo. Sababu tu mimea ya ndizi, migomba, huwa mirefu na migumu kiasi, huonwa kama ni miti ya kweli, wakati ukweli ni kwamba; kutokana na muundo wa sehemu zake za ndani ya shina migomba si miti ya kweli.
Mimea mingi ya aina hii, kitaalamu pseudostem, huweza hata kufikia urefu wa mita 2 – 8, na majani yake hata mpaka urefu wa mita 3.5. na ikikomaa, migomba hutoa mikungu ya ndizi zenye rangi ya kijani ambazo zikiiva hubadilika na kuwa na rangi ya manjano au wakatimwingine hata rangi nyekundu. Kasha kutoa matunda, mgomba hufa na nafasi yak e hu;chukuliwa na mgomba mwingine.
Ndizi hukua kwenye mrindikano mdogo, ujulikanao kama kichana, na kila kichana huwa na ndizi kama 20 hivi huku mkungu mmoja ukuweza kuchukua vichana 3 – 20 kwa wastani. Mkungu unaweza kufkia uzito wa kilo 30 – 50. Ndizi moja kwa wastani huwa na uzito wa gramu 125, ambayo kwa makadirio huwa na maji 75% na mada kavu 25%. Kila ndizi huwa na ganda yenye sehemu laini iliwayo ndani yake. Tena sehemu hiyo ya ndani na maganda huweza kuliwa katika hali ya ubichi au kasha kuiva.
Kwa taratibu nyingi za Magharibi, sehemu ya ndani ikiwa mbichi ndiyo hupendelewa kupikwa na kuliwa, huko huko Asia ndizi na maganda yake hupikwa na kuliwa. Tunda la ndizi huwa na nyuzi nyuzi ndani yake, ambazo huwa hasa katikati ya ganda na sehemu laini ya ndani. Sehemu ya laini ya ndani kwa kawaida hugawanyika kwa urahisi kuanzia juu mpaka chini, kwenye sehemu tatu. Ndizi ni chanzo kizuri cha vitamini B6, vitamini C na potasiamu. Ndizi aina ya Cavendish ndio hulimwa kwa wingi.
Ndizi hulimwa katika zaidi ya nchi 107 duniani. katika nchi nyingi, ndizi humaanisha zile laini na tamu ambazo huliwa kama matunda baada ya mlo. Lakini pia ndizi zawezwa kukatwa na kukaushwa na kuliwa kama vile chipsi.
Ndizi zilizokaushwa pia zaweza kusagwa na kupata unga wa ndizi. Ingawa baadhi ya aina ya migomba ya mwituni huwa na ndizi zenye mbegu kubwa na ngumu, ndizi zinazoliwa kwa kawaida huwa hazina mbegu. Kwa kawaida ndizi zote aidha hutumiwa zikiwa zimeiva, za njano na laini au zikiwa mbichi yaani, za kijani na ngumu kiasi.
Kwa wastani ndizi zinazouzwa biashara kimataifa ni asilimia 10 – 15 tu, huku Marekani na Uingereza wakiwa wanunuzi wakuu.
Kitaalamu ndizi huwekwa kwenye jenasi ya Musa katika familia ya Musaceae, kwenye oda ya Zingibrales.
Mmea wake usio mti kamili, huwa na urefu wa mita 6 – 7.6. Majani yake hukua kuzunguka mmea na hufikia urefu wa mita 2.7 kwa urefu na sentimita 60 kwa upana. Mgomba ndiyo mmea mkubwa zaidi kuliko mimea mingine ya jamii yake. Majani yake huwa makubwa sana na huchanwa kwa urahisi sana na upepo.
Ua moja la kiume huzalishwa na kila mgomba, japo aina nyingine huweza hata kuzalisha matano ya aina hiyo mfano huko Ufilipino. Maua ya kike huzalishwa juu kabisa mwa shina na baadae hukua na kuwa tunda bila hata ya kurutubishwa. Na katika aina nyingi mbegu zimekuwa dhaifu na haziwezi tena kuzalisha mmea mwingine.
Ndizi ni zao linalolimwa katika ukanda wa tropiki na hutumika kwa ajili ya kupikia na kama matunda. Vilevile ndizi huweza kutengenezea starch, chips, pombe (mbege), ama kukaushwa na kuuzwa kama matunda yaliyokaushwa.
Wakati mwingine ndizi hutumika kutengenezea unga ambao huweza kutumika kwenye supu, mikate, ugali na uji. Maua ya ndizi huweza kutumika kama mboga, ila ni lazima yachemshwe kwenye mji ya chumvi ili Kuondoa ladha ya uchungu.
Majani ya mmea huu ni chakula kizuri cha kuku na wanyama na huwa na virutubisho aina ya protein kwa wanyama hawa. Pia majani haya hutumika kwa ajili ya kupakia vitu mbalimbali na kwa ajili ya kuezekea nyumba. Pia ni mazuri sana kwa kutandazia shamba ama bustani. Halikadhalika migomba hutumikla kuzuiya ama kupunguza kasi ya upepo.
MAHITAJI YA MAJI, HALI YA HEWA NA UDONGO
Wakulima wa mwanzo kabisa wa ndizi walitokea huko Maleshia na kusini mashariki mwa bara la Asia. Huko ndizi ilikuwa ikilimwa kwenye udongo wenye rutuba nyingi sana na udongo wa volkano. Pia kwenye delta za mito na kandokando ama ndani ya misitu ambako udongo huwa na rutuba sana. Ndizi hukua vizuri sehemu zenye joto kidogo na unyevu nyevu na mwinuko wa 0-1800 m kutoka usawa wa bahari . Aina nyingine kama ‘DWARF CAVENDISH’ huweza kusitawi hadi kwenye mwinuko wa mita 2100 kutoka usawa wa bahari (sehemu za milimani sana).
Mahitaji ya mvua ni ya wastani wa 1000mm kwa mwaka japokuwa migomba husitawi vizuri kama ikipata maji ya kutosha. Hii ni pamoja na kumwagilia kipindi cha kiangazi bila kutuamisha maji. Halijoto ya 27°C hadi 38°C ndio ifaayo kwa kilimo cha ndizi na migomba hudumaa kama kuna baridi sana (chini ya 13°C.)
Upepo mwingi ni tatizo kwa migomba kwa kuchana majani na kuyaharibu pia kuangusha migomba. Kupanda migomba kwa vikundi husaidia kuzuia upepo na ikibidi migomba iliyobeba ndizi iwekewe nguzo kama zinapatikana.
Udongo mzuri kwa kilimo cha ndizi ni tifutifu yenye uwezo wa kupitisha maji na hewa kwa urahisi. Udongo wenye mbolea nyingi ni mzuri sana kwa migomba.
Ndizi hupandwa kwa kutumia vichipukizi ama migomba midogo ama sehemu za viazi zenye uwezo wa kutoa vichipukizi. Uzao wa ndizi hutegemea sana aina na umri wa vichipukizi vilivyotumika wakati wa upandaji. Vichipukizi vizuri ni vile vilivyochongoka vyenye urefu wa sentimeta 75 na upana wa chini ya shina wa sentimeta 15 na majani yake yamechongoka. Hivi huzaa baada ya miezi 18 tangu kiypandikizwa. Vipandikizi hutoa ndizi hata baada ya miaka 2-3. Migomba mikubwa wastani huzaa bada ya miezi 5-8. Vichipukizi maji vyenye majani mapana havifai kwa kupandikiza kwani huzaa ndizi ndogo na uwezekano wa kupona baada ya kupandikizwa ni mdogo.
Miche ama vichipukizi vya migomba vipandwe kwenye shimo lenye urefu wa sm 60 na upana wa sm 60. Udongo uchanganywe vizuri na mbolea ya kutosha. Kama mvua hazitoshi, shimo liwe na urefu wa sm 150 na upana wa sm 100.
NAFASI
Kwa aina za migomba midogo nafasi kutoka mmea hadi mmea iwe mita 3, na kutoka mstari hadi mstari iwe mita 3. Migomba 1000 kwa ekari. Kwa aina ndefu. Mmea hadi mmea mita 3 na mstari hadi mstari mita 4. Migomba 480 kwa ekari.
MUDA WA KUPANDA MIGOMBA
Muda muafaka ni mwisho wa msimu wa kiangazi ama mwanzo wa msimu wa mvua.
MCHANGANYO WA MAZAO
Mazao kama kahawa, mahindi, mbogamboga, papai, miti ya matunda, kivuli na mbao, na mikunde kunde.
MATUNZO
Wiki 4-6 tangu migomba ipadwe, inapaswa kupaliliwa. Pia migomba inafaa kupangiliwa kwa mafungu. Migomba isizidi minne kwa kila kifungu. ‘KISUMU’, vichipukizi vyote viondolewe kubaki na mgomba mmoja mkubwa, na midogo mitatu yenye ummri tofauti tofauti ili kupata mazao mwaka mzima.
Migomba mingi sana husababisha kuzaa ndizi ndogo. Vichipukizi vyenye afya ndio vibakishwe, Uchaguzi ufanyike kufuata nafasi iliyopo. Vichipukizi visivyotakiwa vikatwe na kuharibiwa sehemu inyokua.
KUTANDAZIA
Matandazo ni muhimu sana na ikibidi yawekwe shamba zima. Matandazo yawekwe umbali wa sm 60 kutoka kwenye kila fungu la migomba. Hii inasaidia Kuepuka wadudu waharibifu kwenye mizizi ya migomba.
MBOLEA
Migomba huhitaji sana mbolea ili izae vizuri. Mimea aina ya mikunde kunde inaongeza rutuba kwenye udongo kama ikipandwa shambani. Pia mbolea ya samadi na mboji ni muhimu sana. Kama kipato kinaruhusu tunashauriwa kutumia mbolea ya miamba ya Minjingu; ‘MINJINGU ROCK PHOSPHATE’ kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha mizizi ya migomba.
MAGONJWA NA WADUDU WANAOSHAMBULIA MIGOMBA
Bacterial wilt (Mnyauko wa bacteria) : Mwanzoni jani mojawapo kati ya majani machanga matatu huanza kuwa njano na kuvunjika. Baadae majani mengine hunyauka na kudondoka kuzunguka shina la mgomba. Ndizi iliyoshambuliwa na ugonjwa huu huwa na madoadoa kwa ndani kama inavyoonekana.
NINI CHA KUFANYA
• Tumia aina zinazostahimili ugonjwa huu kama zipo.
• Tumia vichipukizi visivyo na ugonjwa huu.
• Ondoa migomba yote iliyoathirika na uiteketeze.
UGONJWA WA VIRUSI (BUNCHY TOP)
Ugonjwa huu huweza kutokea wakati wowote wa ukuaji wa migomba.
Huenezwa na aphids na hushambulia hata vichipukizi. Mimea iliyoathiriwa huweza kushindwa kuzaa na ama ikizaa huzaa ndizi ndogo na ngumu.
NINI CHA KUFANYA
• Tumia vichipukizi visivyo na ugonjwa huu.
• Ondoa kabisa migomba yenye dalili za ugonjwa huu, pamoja na viazi vyake na teketeza.
• Thibiti aphids ambao ndio waenezaji.
MAGOJWA YA FANGASI MICHIRIZI MEUSI (Black leaf streak )
Ni ugonjwa hatari sana wa migomba na unashambulia majani ya ndizi. Vimelea vya ugonjwa huu husambazwa na upepo na hukua vizuri kwenye hali ya unyevunyevu. Sehemu za pembezoni mwa jani huanza kukauka na hatimaye jani zima hufa.
Ugonjwa huu husababisha mazao duni na ndizi kuiva kabla ya kukomaa.
NINI CHA KUFANYA
• Ondoa na haribu kwa moto majani yaliyoathirika. Vinginevyo ondoa majani yaliyoathirika na weka mbali na shamba la migomba ama fukia chini sana.
• Epuka kumwagilia majani kwa juu, tunashauriwa kumwaga maji kwenye shina.
• Epuka kupanda kwenye msongamano.
UGONJWA WA PANAMA (Fusarium wilt).
Huu ni ugojwa utokanao na fangasi waishio ardhini na hushambulia mizizi na kuziba njia za kusafirisha maji na madini kwenye mmea, kwa hiyo mmea hunyauka na kufa. Majani huwa ya njano na hatimaye kukauka.
NINI CHA KUFANYA
• Tumia migomba inayostahimili huu ugonjwa kama Dwarf Cavendish.
• Kusafisha shamba na Kuondoa visiki vilivyo shambani huweza kusaidia kupunguza ugonjwa huu.
• Majivu yanaweza kuwekwa kuzunguka
(UGONJWA WA MUOZO SIGARA) THE CIGAR END ROT DISEASE
Ugojwa huu unaweza kuathiri matunda ya ndizi yaliyoiva, na kusababisha kuoza na kukauka kwa ndzi kuanzia mwisho. Palipoathirika huwa na ungaunga kama majivu. Huonekana kama sigara ilyozimwa. Ugojwa huweza kuendelea hadi wakati wa kuhifadhi ama kusafirisha. Huweza kuharibu mkungu mzima na kusababisha hasara kubwa.
NINI CHA KUFANYA
• Zingatia usafi shambani.
• Epuka kujeruhi ndizi na usikate ua la ndizi wiki 8-11 tangu izae.
ANTHRACNOSE
Huu ni ugonjwa unaoshambulia ndizi baada ya kuvuna, hasahasa wakati wa kuhifadhi na kusafirisha. Madoa madogo ya kahawia ama jeusi huanza kutokea kwenye ndizi. Mara nyingi hushanbulia ndizi zilizokomaa vizuri. Hushamiri vizuri kukiwa na hali ya unyevunyevu
NINI CHA KUFANYA
• Hakikisha usafi shambani
• Punguza kujeruhi ndizi
• Ziweke ndizi kwenye maji ya moto 50° kwa dakika 5.
• Kunyuzia mafuta ya jatrofa yaliyochanganywa na maji huzuia anthracnose hadi siku 12.
Zao la ndizi ni miongoni mwa mazao muhimu yanayolimwa hapa nchini. Zao hili la ndizi hutokana na migomba na lina faida nyingi na kubwa katika maisha na ustawi wa maendeleo ya wananchi kiuchumi. Kijiografia, migomba hulimwa na kustawi sana katika ukanda wa tropiki.
Mikoa ya Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Kigoma, na Pwani ni miongoni mwa maeneo ambayo wananchi wake wanalima zaidi zao hili kwa ajili ya chakula na biashara.
Hata hivyo, migomba kwa ajili ya ndizi, inapandwa na kustawi pia katika mikoa mingine nchini, ikiwemo ya Dar es Salaam, Mwanza, Ruvuma, Shinyanga, Lindi, Dodoma, Singida, Katavi, Rukwa na kadhalika. Zao la ndizi ni moja kati ya mazao ya kibiashara ambalo kilimo chake kinaweza kumwinua mkulima kiuchumi endapo kitalimwa kwa kufuata masharti na kanuni bora za uzalishaji wake. Wataalamu wa kilimo cha zao hili, wanashauri kwamba upandaji wake unapaswa kuzingatia aina bora ya migomba, inayozaa ndizi zinazotambulika katika masoko ya ndani na kimataifa.
Migomba ya mwanzo kabisa kustawishwa hapa nchini, mbegu zake zilitokea katika nchi za Malaysia, India na Kusini Mashariki mwa Bara la Asia. Katika nchi hizo, migomba ilikuwa ikistawishwa kwenye udongo wenye rutuba nyingi na udongo wa volkano. Aidha, migomba ililimwa kwenye maeneo ya delta za mito na kandokando au ndani ya misitu, ambapo udongo wake huwa na rutuba nyingi. Mimea hii hustawi vizuri katika maeneo yenye joto kidogo pamoja na unyevunyevu kwenye mwinuko wa nyuzi 0-1,800 kutoka usawa wa Bahari.
Kuna aina mbalimbali za migomba inayostawi kulingana na mazingira tofauti ya hali ya hewa. Kwa mfano, migomba aina ya ‘Dwarf Cavendish’ husitawi hadi kwenye mwinuko wa mita 2,100 kutoka usawa wa Bahari (sehemu za milimani).
Aidha, aina hiyo ya migomba huhitaji mvua ya wastani wa milimita 1,000 kwa mwaka, ingawa pia aina hiyo ya migomba huweza kusitawi vizuri kama ikipata maji ya kutosha zaidi ya hapo. Watafiti wa masuala ya migomba wanaeleza kwamba mmea huo unahitaji hali ya hewa yenye halijoto ya nyuzi za sentigredi kati ya 27 na 38. Kwa mujibu wa watafiti hao, katika maeneo yenye wastani wa nyuzi za sentigredi chini ya 13, mimea hiyo huweza kudumaa na kushindwa kabisa kustawi.
Kwa hapa nchini aina ya migomba inayostawi katika maeneo mengi inajulikana kwa jina la kitaalamu la ‘Musa Balbisiana.’ Asili hii ya migomba ni nchini India. Aina nyingine inayostawi pia hapa nchini inajulikana kwa jina la ‘Musa Acuminata’ ikiwa na asili ya Malaysia. “Kilimo cha migomba kiliingia barani Afrika katika karne ya tano kutoka Malaysia na India,” zinaeleza baadhi ya ripoti za kitafiti.
FAIDA YA ZAO LA NDIZI
Kilimo cha migomba kina faida nyingi sana katika maisha ya mwanadamu. Baadhi ya faida hizo ni pamoja na chakula, biashara, kutengenezea pombe, chakula cha mifugo, kutengenezea mbolea (mboji), kutoa kivuli, kutoa nyuzi, kutengenezea vitu vya sanaa (urembo), kamba, malighafi ya kutengeneza vyakula na vinywaji mbalimbali.
Faida nyingine ambazo zinatajwa na watafiti wa zao hili, ni pamoja na kutumika kama dawa, kuezekea nyumba, kutengenezea makangale (Banana), poda (Powder), chenge (chips), Jeya (flakes), Juisi, Lahamu (jam), vinywaji baridi kama vile juisi ya ndizi, mvinyo (wine) na pombe kali ya kienyeji. Wakati mwingine ndizi hutumika kutengenezea unga unaoweza kutumika kwenye supu, mikate, ugali na uji. Maua ya ndizi huweza kutumika kama mboga, ila ni lazima yachemshwe kwenye mji ya chumvi, ili kuondoa ladha ya uchungu.
Majani ya mmea huu ni chakula kizuri cha kuku na wanyama, na huwa na virutubisho aina ya protini kwa wanyama. migomba hutumikla pia kuzuia ama kupunguza kasi ya upepo.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Mstaafu, Fabian Massawe, aliwahi kuiambia FikraPevu akisema: “Kilimo cha migomba ni mkombozi mkubwa katika uchumi wa mwananchi wa mkoa huu. Ni zao linalotumika na kupendwa na watu wa ndani na hata mataifa ya nje.”
Ili kuweza kunufaika zaidi na kilimo cha zao hili la ndizi, lazima uzalishaji wake uwe wenye ubora wa hali ya juu kwa kufuata maelekezo ya kitaalamu, yanayotaka migomba kustawishwa kwenye ardhi yenye rutuba ya kutosha, shimo lenye kina kirefu na ardhi isiyotuamisha maji kwa muda mrefu. Aidha, migomba inahitaji udongo wenye virutubisho vya kati ya pH5 na pH 8.
Ndizi kwa ajili ya chakula zinaweza kuandaliwa kwa njia tofauti kama vile kuchemsha, kuchoma, kukaanga au kupikwa kwa kuchanganywa na nyama au maharage. Aina ya ndizi zilizozoeleka sana katika maeneo mbalimbali hapa nchini ni pamoja na mzuzu, mshale, matoke, bokoboko, mkono wa tembo na nyingine zinazotumiwa kama matunda mfano kisukari, kimalindi, mzungu na mtwike.
Kwa sasa ndizi zinazolimwa hapa nchini na zinazofahamika kwenye masoko ya kimataifa kutokana na ubora wake ni pamoja na Grand Naine, Williams, Pazz, Jamaica, Uganda green, Gold Finger, Embwailuma Giant na Chinese Cavendish.
Maandalizi ya Shamba Wakati wa kuandaa shamba, mkulima anashauriwa kusafisha sehemu ya shamba lake kwa kutumia zana zozote zinazostahili. Anapaswa kung’oa visiki vyote na mizizi yake yote, kulima sehemu hiyo kwa kutumia jembe la mkono, rato au trekta ili kuwezesha mizizi laini ya migomba kupenya ardhini kwa urahisi.
Baada ya visiki na magugu yote kuondolewa, hivyo ardhi kuwa wazi, inafuata kazi ya kuchimba mashimo ya kupandikiza machipukizi au miche ya migomba. Mashimo hayo yanatakiwa kuchimbwa kwa nafasi inayoshauriwa na wataalam kati ya shina moja la mgomba na jingine. Kwa mujibu wa wataalam hao, inapendekezwa nafasi kati ya mgomba mmoja na mwingine iwe ni mita 2.75 kwa 2.75 kwa migomba mifupi kama vile kimalindi na kisukari.
Katika kila hekta moja, inashauriwa kupandwa mashina ya migomba 1,331, kwa umbali wa mita tatu kwa tatu kati ya mgomba mmoja na mwingine kwa aina ya migomba mirefu na yenye urefu wa kati.
Kwa migomba aina ya Jamaica na Mshale, kila hekta moja inatakiwa ipandwe migomba 1,110 kwa nafasi ya kati ya mita 3.6 kwa 3.6, wakati migomba aina ya Uganda green yanatakiwa mashina 760 kwa hekta moja na kwa nafasi hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, Kagera, Profesa Anna Tibaijuka (CCM), ni miongoni mwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, wanaohimiza ujenzi wa soko la kisasa la ndizi kwa ajili ya mahitaji ya wakulima wa zao hilo, ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira kwa jamii.
CHANGAMOTO YA KILIMO CHA MIGOMBA
RUTUBA YA UDONGO KUPUNGUA
Hii inatokana na kustawisha migomba katika shamba lile lile mwaka hadi mwaka bila kuongeza mbolea ya aina yoyote, hasa mboji na samadi. Mvua zinazonyesha huondoa udongoni vyakula vya migomba. Upandaji wa aina mbalimbali za mimea katika shamba moja huondoa aina mbalimbali za vyakula vya migomba.
MABADILIKO YA HALI YA HEWA
Migomba huhitaji sana maji. Kwa bahati mbaya siku hizi mvua hazinyeshi kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma. Hii ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na uteketezaji wa misitu ya asili na misitu ya kupanda. Matokeo yake ni migomba kukosa maji ya kutosha. Mbali na tatizo hili, upepo mkali na mvua za mawe huharibu mashamba mengi ya migomba.
WATU WENYE UWEZO KUTOKUFANYA KAZI ZA SHAMBA
Kuna vijana wengi wanaomaliza elimu ya msingi kila mwaka, huku taifa na wazazi wao wanategemea warudipo majumbani wasaidie wazazi wao kwa kushiriki kutunza mashamba yao. Lakini hii sivyo ilivyo kwa siku hizi, nguvu yao ya kazi za shamba imepungua sana na wengi wa wazee hao wamezeeka sana na afya zao sio nzuri. Matokeo yake ni kuwa familia nyingi zimezungukwa na mashamba ya migomba na kahawa yasiyotoa tena mavuno mazuri.
WANYAMA WAHARIBIFU
Katika baadhi ya vijiji lipo tatizo la wanyama waharibifu mfano nguruwe (ambao huharibu mashina ya migomba) nyani na tumbili ambao hula matunda ya migomba. Tatizo hili ni kubwa katika sehemu mbalimbali za nchi yetu zinazostawisha migomba kwa wingi.
KUTOJUA KANUNI ZA KILIMO CHA KISASA
Wakulima walio wengi, hawajui kanuni za kilimo cha zao la migomba, yaani kulima kwa kitaalamu. Kwa mfano wakulima wengi hawajui namna ya kudhibiti vifukusi vya migomba na magonjwa mengine.
UPUNGUFU WA ARDHI INAYOFAA
Siyo kila sehemu ya ardhi inaweza kustawisha aina muhimu za migomba kwa wingi na kwa urahisi. Sehemu nyingi zinazofaa sana kwa kustawisha migomba ni zile ambazo kwa sasa zinastawisha zao hilo. Kwa bahati mbaya au nzuri, sehemu hizo zina watu wengi mno kwa kila eneo la kilometa ya ardhi na tayari kuna upungufu wa ardhi kwa ajili ya upanuzi wa kilimo.
Hii ina maana kwamba uzalishaji wa ndizi nyingi zaidi hauwezi kufikiwa kwa kuongeza maeneo ya migomba (maana ardhi haipo) bali kwa kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
Hakuna utaratibu maalumu wa kuuza ndizi kama ilivyo kwa mazao mengine kama vile kahawa, tumbaku, pareto, nafaka na kadhalika yanayoshulikiwa na vyama vya ushirika na bodi za mazao.
USAFIRISHAJI MBAYA
Tatizo lingine linalokabili kilimo cha migomba ni usafiri mbaya katika baadhi ya vijiji na wilaya hasa vilivyo mbali na miji ambayo ndiyo yenye wanunuzi wengi.
Utafiti kuhusu mbinu mbalimbali za kustawisha migomba pia ulidharauliwa kwa muda mrefu ukilinganisha na mazao makuu mengine, hasa yale yanayojulikana kama mazao ya biashara. Hii imesababisha zao hili libaki nyuma kiutafiti na matokeo yake ni kuendelea kukumbwa na matatizo ambayo yangetatuliwa mapema
0 comments: