Email Shafii.ismail09@gmail.com
WhatsApp /CALL 0683308173
WEBSITE http://www.kilimoniuhaiblog.blogspot.com
KUBEBESHA
Ubebeshaji maana yake ni uunganishaji wa sehemu mbili au zaidi za mimea tofauti na kuwa mmea wenye shina moja.
Ubebeshaji hufanyika katika mimea ya mazao ambayo yako katika jamii au ukoo mmoja kwa mfano; embe dodo na viringe, chungwa na limao, parachichi aina ya hass na la kienyeji, passion zambarau na njano, biringanya za aina tofauti, maua ya waridi ya rangi tofauti n.k
Faida za ubebeshaji
- Kuharakisha uzaaji wa matunda miaka 21/2 – 3 ukilinganisha na upandaji kwa kutumia mbegu ambazo huchuka hadi miaka 10 kuanza kuzaa.
- Kudhibiti magonjwa na wadudu walioko udongoni kwa kutumia mashina yanayoweza kustahimili mashambulizi ya visumbufu vya mimea.
- Kuzalisha miti ya matunda yenye vina saba sawasawa na miti mama (mother plant) uliotoa vikonyo.
- Ubebeshaji hufanyika katika miti ya matunda isiyotoa mbegu na ambayo haiwezi kuzalishwa kwa pingili.
- Kuzalisha matunda tofauti katika mti wa matunda mmoja, mfano katika shina la limao linaweza kuzaa machungwa, ndimu na chenza.
- Kuvumila ukame: kwa kuchagua shina la mmea unaovumilia ukame unaweza kuzalisha matunda ambayo sio stahimilivu wa ukame.
- Ubebeshaji unaweza kutumika katika shughuli za kiutafiti kwa kuangalia magonjwa yanayosababishwa na virusi.
- Kupunguza urefu wa miti ya matunda hivyo hurahisisha uvunaji, upogoleaaji wa matawi na upigaji dawa ya kuzuia visumbufu vya mimea.
Vifaa vitumikavyo katika ubebeshaji
- Visu vikali (budding or grafting knives) hivi hutumika katika kukata wakati wa ubebeshaji.
- Mikasi (scateurs) iko mikasi maalumu kwa ajili ya kukatia vikonyo (scions) na vishina (root stock).
- Jiwe la kunolea (sharpening stone) hutumika katika kunolea visu.
- Mikanda ya nailoni (typing strips) hutumika katika kufungia sehemu iliyo unganishwa kwa muda wa wiki mbili (2) hadi tatu (3).
- Nta- hupaka sehemu iliyofungwa ili maji yasisimame ili kuozesha kidonda.
Aina za ubebeshaji
Zipo aina kuu mbili za ubebeshaji
- Ubebeshaji juu ya shina (tip graft).
- Ubebeshaji pembeni ya shina (side veneer)
Uchaguzi wa vikonyo (bud-wood)
- Tawi zuri la mti mama lenye vikonyo vizuri ndio hukatwa na baada ya kuunganishwa ndio huzaa tunda.
- Vikonyo vizuri ni muhimu viwe na vijicho (buds) vilivyoanza kuchomoza na vyenye afya nzuri pia viwe na vijicho zaidi ya vitatu.
- Katika vikonyo mara nyingine unaweza kukuta vijicho vya aina mbili, vile vya maua na vile vya matawi hivyo chagua vile vya matawi ambavyo huwa vimechongoka nchani (vegetative buds) na virefu kiasi.
- Chagua mti mama kwa ajili ya kukata vikonyo vyenye afya nzuri na mti usio na dalili ya mashambulizi ya magunjwa na wadudu.
- Kikonyo kitoke katika mti mama ambao una sifa zinazotakiwa na wateja au mwenye shamba kwani hatimae ndicho kitakacho toa matunda yenye sifa zilezile za mti mama.
- Kwa miti ya matunda kikonyo/vikonyo vitoke kwenye mti mama ambao tayari unazaa na watu wanayapenda matunda yake na ubora unaotakiwa.
- Vikonyo vinavyotumika ni vile vya msimu uleule (current season wood) au msimu uliopita (previous season wood) usitumie vikonyo vilivyo zeeka au kukomaa sana.
Mambo ya kuzingatia katika ubebeshaji
- Usafi; vifaa vyote vitakavyotumika katika ubebeshaji lazima viwe safi, visu, mikasi, kamba za kufungia “labels” n.k
- Vikonyo vinavyotumika ni muhimu viwe vimeandikwa aina ya miti ama (variety) ili kusiwe na uchanganyaji wa majina.
- Mikono ya mbebeshaji lazima iwe safi wakati wote wa shughuli za ubebeshaji ili isije ikachafua sehemu ya ungio na kusababisha kuoza.
- Sehemu ya ungio ifungwe vizuri ili maji yasije yakapenya na kuozesha sehemu hiyo.
- Mwagilia maji kwenye shina mara kwa mara ili kikonyo kiweze kuchipua kwa haraka.
- Ubebeshaji ufanyike wakati shina likiwa katika hali ya kukua kwa kasi na vikonyo vikiwa katika hali ya kujiandaa kuchipua.
- Mara nyingi kamba za nailoni ndizo hutumika katika kufunga ungio kwa sababu haziozi kirahisi na huzuia maji yasipenye kwenye kidonda cha ungio.
- Visu na mikasi vinavyotumika katika ubebeshaji lazima vinolewe na viwe vikali sana ili kufanya mikato safi na inayotakiwa (clean and sharp cuts).
- Muunganiko wa kikonyo na shina huwa tayari baada ya vikonyo kuanza kuchipua na mara nyingi baada ya wiki tatu hadi miezi miwili.
Aina mbili za ubebeshaji
Ubebeshaji wa juu ya shina (tip grafting)
- Katika aina hii ya kwanza shina hukatwa sehemu ya juu na kubakia kisiki ambacho huunganishwa na kitawi cha mti mama (scion) ambacho baadae huzaa matunda.
- Shina kazi yake ni kusafirisha maji na virutubisho kutoka kwenye udongo na kupeleka kwenye kikonyo
Vile vile shina hubeba sehemu ya juu ya mmea mzima pamoja na ile inayozaa matunda hivyo basi unene wa kikonyo na shina ni vizuri vilingane au shina liwe nene kuliko kikonyo au kitawi.
- Shina likiwa jembamba kuliko kikonyo mara nyingi mti huo huvunjika sehemu ya ungio wakati unapoanza kuzaa, haliwezi kustahimili uzito wa juu.
Uunganishaji wa pembeni ya shina (side grafting) Uunganishaji wa aina hii hutumia kikonyo (kitawi) au kijicho kimoja toka kwenye kikonyo (bud) kikonyo hichi chenye macho mengi huitwa (bud stick)
- Kikonyo kimoja huwa na macho mengi kwa hiyo kwa kutumia kijicho kimoja kimoja huwa ni njia nzuri ambayo haiharibu sana mti mama kwa kukata kata vikonyo vingi.
Njia mbalimbali za ubebeshaji
Njia hizi zimepewa majina ya kitaalam kufuatana na mikato mbalimbali inayokatwa kwenye kikonyo. Kijicho au kishina. Njia hizi ni kama zifuatazo:-
- Cleft grafting. Njia hii huitwa kulingana na shina kupasuliwa kutoka sehemu ya juu kuelekea chini kiasi cha sentimita 21/2 hadi 3 hivyo mpasuko huu hufanana na kwato za ng’ombe au mbuzi. Njia hii hutumika wakati kikonyo na shina hulingana unene kiasi cha unene wa kalamu ya risasi.
- Wedge grafting. Njia hii hutumika wakati mikato ya vikonyo huwa kama chimbuo la mashimo. Sehemu hii ya chini ya kikonyo huchongwa pande mbili ana kuacha ikiwa imechongoka kama chimbuo. Sehemu hii ndio huingizwa au kuchomekwa sehemu ya shina iliyopasuliwa.
- Whip/tongue grafting. Njia ya ulimi hutumika kubebesha miti iliyo na vishina vyembamba hivyo mkato mfano wa ulimi hukatwa kwenye shina na kikonyo ili kupata muunganiko ulio imara.
- Splice or whip grafting. Mkato huu mshaziri hukatwa kwenye sehemu ya juu ya shina na sehemu ya chini ya kikonyo na baadae kuoanisha sehemu hizi mbili. Hutumika wakati shina na kikonyo vina unene sawa hutoa muunganiko mzuri.
Ubebeshaji wa kijicho (budding)
Kuna njia au namna mbalimbali za ubebeshaji wa aina hii ambazo pia zimepewa majina kulingana na mikato katika shina au kijicho.
Njia hizo ni kama zifuatazo;
- T au budding. Mikato katika shina hufanana na herufi T ya kawaida au ya wima au iliyogeuzwa.
- Rind budding. Ganda lenye jicho (bud) huondolewa na kupachikwa sehemu ya shina ambayo ganda lake lenye ukubwa huohuo limeondolewa.
- Chip budding. Kijicho pamoja na kipande cha mti hubebeshwa katika kishina chenye unene kiasi na ganda la kishina likiwa limeshikamana na mti na sio rahisi kuachanisha.
- Forket budding. Hutumika kuunganisha miti yenye utovu mwingi na maganda ya shina ni manene
Sababu za shina na kikonyo au kijicho kushindwa kuungana
- Shina au kikonyo huwa na viini au vimelea vya ugonjwa
- Mimea kutofautiana kwa kiasi kikubwa katika jamii
- Kutokuzingatia usafi wakati wa kuunganisha
- Kutokuzingatia msimu au wakati wa uunganishaji
- Ufungaji mbaya sehemu ya kiungio (union)
- Matunzo mabaya mfano kutomwagilia maji
http://www.kilimoniuhaiblog.blogspot.com
0 comments: