Thursday, 8 June 2023

KILIMO CHA CHOROKO

 Email Shafii.ismail09@gmail.com 

WhatsApp /call 0683308173 

Website http://www.kilimoniuhaiblog.blogspot.com

Choroko ni zao la chakula na biashara lenye kiasi kikubwa cha protini na madini ya phosphorus na calicium. Zao hili likilimwa vizuri hutoa mavuno kati ya Kg 400 hadi 900 kwa ekari.

Udongo na hali ya hewa 
 Choroko hustawi katika udongo wa aina tofauti tofauti usiotuamisha maji. Hulimwa kutoka mita 0 hadi 1500 kutoka usawa wa bahari japokuwa kuna mbegu nyingine zinaweza kukubali zaidi ya ukanda huu.Hili ni zao linalostahimili ukame.

Aina za Choroko
Kuna aina kuu mbili za choroko ambazo pia zimegawanyika katika makundi mawili,choroko nyeusi na choroko za kijani.

Choroko zinazotambaa , hizi ni choroko ambazo zinarefuka sana na hutambaa sehemu mbalimbali.
Choroko zinazosimama, hizi ni choroko ambazo zinakuwa kwa kusimama kwenda juu.

Kipindi kizuri cha upandaji wa choroko
Choroko hazihitaji maji mengi hivyo ni budi zipandwe mwishoni mwa msimu wa mvua, Pia zinaweza kupandwa katika shamba lililolimwa mpunga.

Nafasi cha upandaji wa choroko na kiasi cha mbegu
Choroko huitaji mbegu kiasi cha kilogram 8 hadi kumi kwa ekari moja.
Panda choroko zako kwa nafasi ya sentimeta 30 mastari na mstari na sentimeta 10 shina hadi shina (30 x10 )sentimeta au (40 x 8 )sentimeta

Samadi na mbolea ya viwanda
Kama shamba lako halina rutuba ya kutosha unaweza kuongeza samadi kiasi cha tani tano kwa ekari na pia unaweza kupanda kwa kutumia mbolea ya NPK kg 50 kwa ekari. Weka mbolea zote kabla ya kupanda.

Umwagiliaji
Kama umepanda kipindi cha ukame sana au unalima kilimo cha umwagiliaji basi mwagilia shamba lako upate unyevu wa kuotesha mbegu, kisha baada ya mbegu kuota kaa siku 6 hadi 10 na umawgilie tena. Mara tatu za kumwagilia zinatosha kwa choroko. Na palilia shamba lako mapema kuzuia magugu kuota ndani ya shamba lako na kwa palizi moja inaweza kutosha.

Magonjwa ya Choroko
yellow mosaic virus ( Ugonjwa wa manjano)
Dalili- mmea unakuwa wa njano na madoa ya njano katika majani.
Kinga na tiba-Panda mbegu zinazostahimili magonjwa.

Powdery Mildew (Ukungu)
Dalili-Majani yanakuwa na vidoti vya njano ambavyo vinabadilika kuwa vya kahawia au kijivu haraka na ambapo kunakuwa na unga unga katika majani.
Kinga na tiba-Panda mbegu zinazostahimili ukungu,Pulizia dawa za ukungu (Fungicide).
anza kupuliza wiki tatu baada ya mimea kuota na kuendelea kulingana na hali halisi.

Leaf spot (Vidoti katika majani)
Dalili-majani yanakuwa na vidoti vya mviringo na visivyo na umbo maalum ambapo katikati  yanakuwa na rangi rangi ya kijivu na weupe na mistari ya rangi ya wekundu-kahawia au nyeusi-kahawia.ugonjwa huu husababisha hasara hadi ya asilimia 58 ya mapato.
Kinga na Tiba-Panda mbegu inayostahimili ugonjwa huu,Choma mabaki ya mimea hii na ile ya jamii moja baada ya kuvuna.Pulizia  dawa za ukungu (Fungicide) Katika nafasi ya wiki mbili mbili kama eneo hilom linashambuliwa mara kwa mara na ukungu.

Wadudu.
Kuna wadudu mbalimbali wanaoshambulia choroko kama vile aphidi,funza wa vitumba,nzi wa maharage.Wazui wadudu hawa kwa kupuliza dawa za wadudu mara tu baada ya mimea kuota,dawa kama karate,twigathoate,dimethote na nyinginezo zinaweza kutumika.

Uvunaji
Mara tuu choroko zinapofikia asilimia 85 ya ukaukaji zinabidi zivunwe ukichelewa zitapukutikia shambani.


http://www.kilimoniuhaiblog.blogspot.com

0 comments: