Pamoja na kuwa na uhitaji mwingi hasa kwa nchi za bara la Asia zikiwamo China, India, Japan, Marekani na pia nchi za Ulaya, bado Watanzania wengi hasa maeneo linapokubali zao hilo, hawajachangamkia fursa ya kulima ufuta.
Wataalamu wanaeleza kuwa hata uhaba wa mafuta nchini ungeweza kuwa historia kwa kulima ufuta kwa wingi.
Wanasema kilo mbili ya ufuta ghafi zikisindikwa zinaweza kutoa lita mbili hadi tatu za mafuta, hivyo Tanzania inahitaji hekta milioni 1.1 za kilimo cha ufuta, ili kukidhi mahitaji ya mafuta.
‘’Wanunuzi wa ufuta ni wengi hivyo kutoa fursa kubwa kwa wakulima, serikali za mtaa na serikali kuu kwa ujumla na hilo hujidhihirisha wakati wa mavuno, ambapo ufuta wote unaozalishwa nchini huuzwa huku bado wanunuzi wakiwa wanahitaji zaidi,’’ ’Uzalishaji wa mafuta ya ufuta nchini ni mdogo sana, ndio maana ni nadra kuyakuta sokoni, ila wananchi wangeamua kuzalisha upatikanaji wa mafuta nchini ungeongezeka.’’
Serikali kupitia kituo cha utafiti wa kilimo cha Naliendele mkoani Mtwara, ina mkakati wa kupeleka mbegu maeneo mbalimbali ili kuongeza uzalisaji wa wa ufuta nchini.
kituo kina lengo la kufanya utafiti utakaosababisha kuzalishwa kwa mbegu inayozalisha ufuta mweupe na wenye mafuta mengi ili kukidhi matakwa ya soko.
Matumizi ya ufuta
Kimatumizi, ufuta unaweza kuuzwa moja kwa moja au kuchakatwa na kutengenezwa vitu mbalimbali yakiwamo mafuta ya kula. Unga wake unaweza kutumika kama uji lishe. Ufuta na mazao yake pia unaweza kutumika kama chakula, kutengenezea keki na bidhaa kama sabuni na vipodozi.
Kilimo cha ufuta
Zao la ufuta linastawi katika maeneo yenye mvua za kutosha kuanzia milimita 600 hadi 800. Linaweza pia kustawi katika mvua za milimita 400 kwa sababu linavumilia ukame kwa kiasi fulani.
Ili kulima kitaalamu, mkulima hana budi kuandaa shamba kwa kupanda mbegu bora. Kuna mbegu za muda mrefu aina ya Ziada inayochukua siku 134 na mbegu ya muda mfupi ya Lindi 2002 inayochukua siku 110. Kwa mikoa ya kusini, kipindi bora cha kuandaa shamba ni mwezi Januari.
Kwa mikoa yenye mvua ndogo kama Dodoma, mbegu bora ni Lindi.
Mbegu nyingine za ufuta ni pamoja na Mtondo 2013, Mtwara, Bora, Naliendele 92, morada, Lindi white, SSBS, SSBS4, SSBS 7 na Zawadi. Hata hivyo, wanunuzi wengi hupendelea Lindi 2000 inayotoa ufuta mweupe. Nafasi za upandaji ni sentimita 10 mmea hadi mmea na sentimita 50 mstari hadi mstari. Mkulima azingatie na kusafisha shamba vizuri na kuwahi kuupunguza ufuta wake kabla haujawa mkubwa.
Udongo unaofaa kwa zao la ufuta ni ule usiotuamisha maji na wenye kiwango cha ‘alkaline’ na ‘acid’ kati ya tano hadi sita,huku ukiwa na rutuba ya kutosha na joto la nyuzi 25 hadi 30.
Ufuta unaweza kulimwa kwa kuchanganywa na mazao mengine kama vile korosho, mihogo na mahindi.
Hata hivyo,unapofanya kilimo mseto, ni muhimu kuyaachia nafasi mazao yako.
Kwa mujibu wa wataalamu, ili kuwe na tija katika mavuno ya ufuta, lazima mkulima asimamie na kuhudumia shamba lake kuanzia palizi, udhibiti wa wadudu na magonjwa na kuvuna kwa wakati.
0 comments: