Email address shafii.ismail09@gmail.com
Msingi wa tatizo la nyanya kuoza kitako
Imekuwa kawaida kwenye kilimo cha nyanya mkulima kuona matunda mengi shambani yameoza sehemu ya kitako, kitu ambacho hufanya nyanya kuwa na ngozi ngumu yenye rangi nyeusi. Hali hii hutokea hasa hasa matunda yanapokuwa mabichi (yanayoendelea kukua) na hata yanapokuwa yameanza kuiva.
Linapoanza tatizo la nyanya kuoza kitako, matunda hutengeneza malenge lenge ya maji (muozo) kwenye kitako ambapo kadri matunda yanapokuwa muozo nao huongezeka ukubwa na kitako hubadilika rangi na kuwa cheusi na baadae hukakamaa na kutengeneza ngozi ngumu nyeusi.
Muozo huu unaweza hata kuathiri nusu ya tunda zima kutokea chini. Na tatizo hili huweza pia kutokea kwenye mazao kama pilipili, matango, nyanya chungu, matikiti na maboga.
Tatizo la nyanya kuoza kitako si ugonjwa bali ni hali ya kifiziolojia inayosababishwa na ama kutokuwepo kwa madini ya chokaa (Calcium, Ca2+) kwenye udongo, au mimea kushindwa kufyonza madini ya chokaa (Calcium, Ca2+) kwenye udongo (kama yapo) au kutokuwepo kwa uwiano sawa wa madini ya chokaa (Calcium, Ca2+) katika sehemu mbalimbali za mmea hasa matunda.
Hivyo basi unatakiwa kuelewa kwamba tatizo hili halisambai kutoka shamba moja kwenda lingine, wala kutoka mmea mmoja kwenda mwingine, wala kutoka tunda moja kwenda jingine. Na hivyo basi hakuna dawa yoyote iwe ya wadudu au ya fangasi inayoweza kutibu tatizo hili.
Nyanya zilizo athiriwa na tatizo la kuoza kitako
Nini hasa kazi ya Calcium (Ca2+) kwenye mmea?
Calcium ni kiungo (kirutubisho) muhimu katika kuta za seli za mmea, hivyo uwepo wake ni muhimu sana kwa ukuaji sahihi wa mmea. Na inapotokea inahitajika kwa wingi kuliko inavyopatikana mengi hutokea; matunda huoza (Mfano; nyanya kuoza kitako), mmea hudumaa, majani machanga hufa kwenye ncha na mizizi kushindwa kurefuka. (4)
Soma zaidi kuhusu kilimo cha nyanya:
- Kilimo bora cha nyanya
- Magonjwa ya nyanya na jinsi ya kuyadhibiti
- Wadudu waharibifu wa nyanya na jinsi ya kuwadhibiti
Visababishi vya matunda ya nyanya kuoza kitako
Kwakuwa tayari tunajua kuoza kitako kunasababishwa na upungufu wa Calcium, hapa tunaangalia sababu zinazopelekea mmea kushindwa kufyonza Calcium (Ca2+) kwenye udongo ambapo baadae hupelekea mmea kukosa au kushindwa kuitumia (Calcium, Ca2+) iliyopo.
- Kutokuwa na ratiba maalumu ya umwagiliaji kwa kuwa mmea unahitaji maji na wakati mwingine unahitaji ukame usio na madhara. Ukame sana au maji ya kutuama muda mrefu hufanya mmea ushindwe kufyonza Calcium (Ca2+) kwenye udongo.
- Kuwepo kwa virutubisho vya Nitrogen kwa wingi sana kwenye udongo. Hii hufanya mmea ukue kwa kasi kubwa kuliko mmea wenyewe unavyoweza kufyonza Calcium, (Ca2+) kwenye udongo
- pH kubwa sana (Zaidi ya 7.0) au ndogo sana (chini ya 6). pH inatakiwa iwe 6.5; isipungue sana wala isizidi sana.
- Udongo kuwa na chumvi chumvi nyingi sana.
- Kuharibika kwa mizizi kutokana na shughuri za ulimaji/palizi shambani.
- Baridi kali sana kwenye udongo hufanya mmea ushindwe kufyonza Calcium, (Ca2+) kwenye udongo.
Jinsi ya Kudhibiti tatizo la nyanya kuoza kitako
Tatizo la nyanya kuoza kitako haliwezi kutibika, na tunachoweza kufanya ni kuondoa au kupunguza tu kwa kiasi sababu zinazochochea kutokea kwa tatizo hili:
- Weka utaratibu maalumu wa umwagiliaji na uufuate. Kama una mwagilia mara mbili kwawiki basi iwe hivyo.
- Hakikisha kuwa udongo wako hautuamishi maji na tumia samadi au mboji ukiweza ili nyanya zipate mahitaji yake muhimu na hivyo upunguze matumizi ya mbolea za nitrogeni.
- Unapotumia mbolea za nitrogeni, tumia mbolea ambazo zina kiwango kidogo cha nitrogeni na utumie viwango vinavyoshauriwa au utumie nusu ya kiwango hicho. Pia mbolea za nitrogeni ziwe na kiwango kingi cha Phosphorus na epuka kuweka mbolea nyingi wakati nyanya zinaanza kutoa matunda.
- Tumia matandazo (Mulch) ili kupunguza kupotea kwa maji kwenye udongo.
- Dhibiti pH ya udongo, na uhakikishe haizidi sana wala kupungua sana kutoka 6.5
- Tumia mbolea ya maji ya Calcium (Ca2+) – Ca foliar fertilizer
- Kita miti ya kupandia mimea ya nyanya (Stakes)
- Epuka kuharibu mizizi wakati wa kulima/kupalilia shambani.
Nini kifanyike nyanya zikishaoza kwenye vitako?
- Chuma au ondoa matunda yote yaliyoathirika na uyatupe, yaliyo athirika kidogo unaweza kukata na kutumia sehemu nzima, hayata kuzuru. Ukisha yaondoa matunda yaliyooza mmea utaweka tena maua na kuzaa matunda mengine, mazuri. (2) (1)
- Pulizia mbolea ya maji ya Calcium baada ya kuondoa matunda yote yaliyoathirika. (2)
Mazingatio muhimu:
Tatizo la nyanya kuoza kitako agahalabu hutokea kwa sababu za kimazingira zaidi na hivyo kufanya lisiwe ndani ya uwezo kulidhibiti kabisa lisitokee.
Na baadhi ya rejea zinasema tatizo hili ni (kama) lazima litokeee katika hatua moja wapo ya uzaaji wa matunda kwenye nyanya ambapo mara nyingi huwa ni ile ya kwanza.
Hata hivyo baadaye tatizo hili huisha lenyewe bila wewe kufanya chochote kulidhibiti (…na pengine bila kusababisha matatizo makubwa sana).
0 comments: