VIRUTUBISHO VITATU MUHIMU
Mmea hutumia virutubisho vikuu vitatu ambavyo huchukua nafasi kubwa katika maendeleo ya mmea. Virutbisho hivyo ni naitrojen (N), fosiforasi (P) na potasiamu (K).
Makala
Fahamu virutubisho vitatu muhimu kwa mimea
Mmea hutumia virutubisho vikuu vitatu ambavyo huchukua nafasi kubwa katika maendeleo ya mmea. Virutbisho hivyo ni naitrojen (N), fosiforasi (P) na potasiamu (K).
MIMea hupata chakula kutoka kwenye udongo. Chakula hicho huitwa virutubisho kwa mmea ambavyo kitaalamu vipo 16, vikiwamo 13 vinavyopatikana kwenye udongo.
Mmea hutumia virutubisho vikuu vitatu ambavyo huchukua nafasi kubwa katika maendeleo ya mmea. Virutbisho hivyo ni naitrojen (N), fosiforasi (P) na potasiamu (K).
Kwa kifupi wengi huita virutubisho hivi kwa kifupi cha N-P-K. Na kila mbolea huandaliwa na kuwekewa asilimia tofauti tofauti ya virutubisho vikuu hivi
Kwa mfano, kuna NPK (17:17:17), CAN (27:0:0), DAP (18:46:0). Hizi ni aina tatu za mbolea zilizoundwa na virutubisho vikuu vitatu kwa mpangilio wa N:P:K na kiwango chake cha asilimia za virutubisho katika mabano.
Chukua mfano wa mbolea ya DAP hap juu. Fosiforasi ipo kwa kiasi kikubwa (46) naitrojeni (18) na potasiamu (0). Hii inamaanisha kuwa hapa fosiforasi ina mahitaji makubwa kuliko virutubisho vingine.
Ndiyo maana wataalamu tunasema udongo una mengi ambayo kama mkulima atayajua na kuyafanyia kazi, ana nafasi kubwa ya kufurahia kilimo.
Hakuna asiyejua kuwa udongo ni muhimu kwa maisha endelevu ya mwanadamu, lakini tayari sehemu kubwa ya bara la Afrika, ikiwamo Kusini mwa jangwa la Sahara kuna tatizo la rutuba ndogo ya udongo.
Tunaposema rutuba ndogo ya udongo ni upatikanaji mdogo wa virutubisho vitatu vya N-P-K vya mmea katika udongo.
Swali; wakulima wafanyeje kuboresha rutuba ya udongo na hatimaye waweze kupata matunda ya shughuli zao za kilimo?
Umuhimu wa Fosiforasi
Mimea hupata virutubisho muhimu kwa ajili ya ukuaji kupitia udongo. Mizizi ya mimea hunyonya maji yaliyoko kwenye udongo yakiwa na virutubisho hivi.
Fosiforasi huchukuliwa na mimea ikiwa tu iko katika hali ya kuyeyuka katika maji yaliyopo kwenye udongo.Kama ilivyo Nitrojeni, fosiforasi pia ni muhimu kwa ukuaji na ustawi wa mazao.Majukumu yake ni pamoja na kusaidia ukuaji wa mizizi, kuharakisha kukomaa kwa mazao (kuchanua, uzaaji wa matunda na mbegu).
Mengine ni kuimarisha ubora wa mazao (hasa mazao ya mboga mboga) na kutengeneza nitrojeni iliyoko hewani kuwa katika hali ambayo inaweza kutumiwa na mimea hasa ile ya aina ya mikunde.
Lini Fosiforasi inahitajika?
Fosiforasi na hata virutubisho vingine hupotea udongoni kwa sababu mbalimbali.
Hivyo, kuna haja ya mkulima kujua muda mwafaka wa kurudisha virutubisho hivyo na njia maalumu zitakazotumika kurudisha virutubisho hivyo.
Kitaalamu, virutubisho hivi vitatu huongezwa udongoni kwa mbolea asili kama samadi au mbolea za dukani kama UREA, DAP na nyinginezo. Lakini pia kuoza kwa majani katika udongo huongeza virutubisho udongoni
Inasikitisha kumuona mkulima mara anapomaliza kuvuna, badala ya kuacha masalio yaoze, anayachoma moto. Hajui kuwa kuchoma moto ni kuondoa virutubisho.
Kiasi cha fosiforasi kinachotakiwa kwa ukuaji mzuri wa mimea kinategemea aina na umri wa mmea. Upungufu wa virutubisho vya fosiforasi hutokea wakati mimea inapokuwa midogo au wakati mizizi bado midogo.
Mmea mdogo unapokuwa haupati fosiforasi ya kutosha, uwezo wake wa kukua utaathiriwa. Hapa ndipo mmea unapodumaa, majani kuwa ya njano au maua kuanguka.
Kwa hiyo ukuaji mzuri wa mizizi ni muhimu ili kuwa na mwanzo mzuri wa ukuaji wa mmea. Mmea mdogo unahitaji fosiforasi kwa wingi wakati unapoanza kukua, kiasi kingine unapoendelea kukua na kiasi kingine kitasaidia wakati wa kuzaa matunda na mbegu
Unawekaje mbolea?
Unaposafisha shamba lako, hakikisha udongo unauchanganya na mbole. Na hata unapoandaa mashimo maalumu weka tena mbolea huku ukimwagilia kwa siku mbili hadi tatu asubuhi na jioni kabla ya kupanda mche.
Kwa kufanya hivi, utajihakikishia upatikanaji wa virutubisho muhimu ikiwamo fosiforasi ambayo ni muhimu katika maisha ya mbegu yako kuelekea kuwa mmea wenye afya.
Mbegu ikishaota, utahitajika kuweka mbolea, wakati wa kukua utaweka mbolea lakini pia wakati wa kutoa maua pia utaweka mbolea.
Kuna aina ya mazao yanayohitaji fosiforasi kwa wingi. Mazao haya ni kama vile mahindi, kabichi, viazi, maharage, na aina nyingine za mikunde.
Pia, kuna mimea mingine yenye uwezo mkubwa wa kutafuta na kuchukua fosiforasi katika udongo. Mimea hii ni kama sukuma wiki, mbaazi na alizeti mwitu.
Vitu vinavyopunguza virutubisho kwenye udongo
Kuna vitu vya aina mbili ambavyo huondoa au kupunguza rutuba ya udongo au kupunguza virutubisho muhimu udongoni.
Vitu vya asili
Mojawapo ya vitu hivi ni mvua ambayo hufanya virutubisho muhimu viende chini zaidi. Lakini pia joto kali na michakato ya kikemia ambayo hutokea katika miamba.
Udongo wa kichanga pia huwa na virutubisho kidogo, kutokana na uwezo wake mdogo wa kuhifadhi maji.
Kazi za binadamu
Upungufu wa fosiforasi katika udongo pia husababishwa na kazi za binadamu na jinsi wanavyohudumia mashamba yao.
Kwa mfano, kulima mazao mengi kwa mfululizo na kuvuna huondoa fosiforasi kwenye udongo. Uhudumiaji mbaya wa mashamba kama vile kuchoma mabaki ya mazao shambani, kutoongeza mboji katika udongo na kulima kunakosababisha mmomonyoko wa udongo vinachangia kupungua kwa fosiforasi katika udongo. Shughuli zote hizi hufanya udongo katika mashamba uchoke.
0 comments: