Tuesday, 23 May 2023

KILIMO CHA MIGOMBA

Kilimo cha migomba kimekuwepo kwa miaka mingi sana hapa Tanzania. Kilimo cha ndizi ni maarufu sana kwa sababu zao la ndizi linatumika kama chakula kikuu kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera, Kilimanjaro na Mbeya na hivyo kulifanya muhimu, kufuatia baada ya mazao ya mahindimpunga, mtama, muhogo, viazi na mazao ya jamii ya kunde kama vile maharage.

Zao la ndizi linaweza kuwa moja kati ya mazao ya biashara iwapo litazalishwa kwa kufuata kanuni za kilimo bora cha migomba na misingi ya kibiashara katika uzalishaji wa migomba.

Hii ni pamoja na kupanda migomba ya kisasa inayozaa ndizi zinazotambulika katika masoko makubwa ya miji mikubwa ndani ya nchi yetu na katika masoko ya kimataifa.

Mazingira Yanayostawisha Migomba

Hali ya hewa

Kiasi cha joto kinachofaa ni nyuzi joto za sentigredi 25 hadi 30. Chini ya nyuzi joto 16 migomba haikui vizuri.

Mvua na mwinuko

Kiasi cha chini cha mvua kifaacho kwa kilimo cha ndizi ni milimita 100 kwa mwezi au 1200mm kwa mwaka. Mwinuko kutoka usawa wa bahari ni hadi mita 1800 juu ya usawa wa bahari. Zaidi ya mwinuko huo migomba haikui vizuri.

Udongo

Migomba hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha, kina kirefu, usiotuamisha maji na pia usiwe na chumvi. Chachu ya udongo inafaa iwe kati ya pH 5 hadi 8.

Maeneo yanayolima migomba

Nchini Tanzania mikoa inayoshughulika na kilimo cha migomba na kuzalisha ndizi kwa wingi ni pamoja na Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Kigoma, na Pwani.

Hata hivyo zao la ndizi linaendelea kuenea katika mkoa mingine nchini ikiwa ni pamoja na Dar es salaam, Mwanza, Ruvuma, Shinyanga na Lindi. Pia Dodoma na Singida.

Kilimo cha migomba kinaweza kufanyika katika kipindi chote cha mwaka kulingana na kiasi na mtawanyiko wa mvua hasa mabondeni au kwa umwagiliaji.

Shamba la migomba
Shamba la migomba

Mbegu za Migomba

Asili ya ndizi

Asili ya migomba ni nchi za Malaysia na India ambazo ziko Kusini Mashariki mwa bara la Asia.

Migomba inayolimwa sasa imetokana na aina ya migomba ijulikanayo kama Musa balbisiana ambayo asili yake ni India, na Musa acuminata ambayo asili yake ni Malaysia.

Kutoka Malaysia na India migomba ilifika Afrika Mashariki katika karne ya tano.

Aina za ndizi

Kuna aina nyigi sana za ndizi. Nchini Tanzania ndizi zinazozalishwa hutofautiana kwa majina kutokana na eneo au mkoa unaozalisha. Hata hivyo zinaweza kugawanywa katika makundi mawili;

  • Kundi la kwanza ni ndizi ambazo huliwa kwa kuzichoma, kukaanga au kupikwa zikichanganywa na vyakula vingine kama vile nyama. Aina za ndizi hizo ni pamoja na Mzuzu, Mshare, Matoke, Bokoboko na Mkono wa Tembo.
  • Kundi la pili ni ndizi zile ambazo huliwa kama matunda, aina hizo ni kama vile Kisukari, Kimalindi, Mzungu na Mtwike.
  • Kuna aina nyingine za ndizi ambazo kwa sasa huzalishwa hapa nchini ambazo zina fahamika kwa ubora wake katika masoko ya ndizi ya kimataifa. Aina hizi ni pamoja na Williams, Grand Naine, Pazz, Jamaica, Gold Finger.
  • Nyingine ni Uganda green, Embwailuma Giant na Chinese Cavendish.

Sifa za mbegu bora za migomba

Mbegu bora ni msingi wa kilimo bora cha migomba. Unapoandaa mbegu za migomba kwa ajili ya kupanda, ni muhimu kuzingatia sifa zifuatazo;

  • Uzaaji wa ndizi. Chagua mbegu ambayo inazaa sana ndizi. Yaani mbegu ya migomba inayotoa mikungu mikubwa yenye ndizi nene.
  • Ukinzani wa magonjwa. Chagua mbegu ya migomba ambayo ina ukinzani mzuri wa magonjwa kama vile mnyauko bakteria, mnyauko fusari, n.k.
  • Mbegu iendane na soko au matumizi yako. Chagua mbegu ya migomba ambayo itaendana na aina ya matumizi yako.

Sifa za chipukizi bora la mgomba

  • Liwe chipukizi sime, yaani lenye majani membamba na siyo chipukizi maji yaani lisiwe lenye majani mapana.
  • Litoke kwenye mgomba (shina) wenye afya nzuri, usiokuwa na magonjwa, minyoo ya mizizi, wala vifukusi vya migomba.
  • Litoke kwenye mgomba wenye sifa ya kuzaa mikungu mikubwa.
  • Liwe na afya nzuri na lisiwe na dalili za ugonjwa, wadudu, au mayai ya vifukusi.
  • Urefu uwe kati ya meta 1 na meta 2. Kipenyo cha sehemu ya chini ya shina la chipukizi (tunguu) kiwe ni kati ya sentimeta 15 hadi 25.

Jinsi ya Kupanda Migomba

Msimu wa kupanda migomba

Msimu wa kupanda migomba ni msimu wa mvua za masika: kuanzia mwezi Machi mpaka mwezi May. Na wakati wa msimu wa mvua za vuli unaweza kupanda kuanzia mwezi Oktoba mpaka Disemba. Kama umeandaa mfumo wa umwagiliaji ili ufanye kilimo bora cha migomba unaweza kupanda migomba karibu wakati wowote ule wa mwaka.

Kuandaa shamba

Safisha sehemu inayohusika kwa kutumia zana ulizonazo. Ng’oa visiki vyote na mizizi yake yote. Lima sehemu hiyo kwa kutumia jembe la mkono, rato, au trekta ili kuwezesha mizizi laini ya migomba kupenya ardhini kwa urahisi.

Baada ya visiki na magugu yote kuondolewa na hivyo ardhi kuwa wazi, uchimbaji wa mashimo ya kupandikiza machipukizi au miche ya migomba unaweza kufanyika.

Uchimbaji wa mashimo ya kupandia migomba

Uchimbaji mashimo inafaa ufanywe mapema kiasi cha juma moja hadi mwezi kabla ya muda wa kupanda migomba.

Shimo lichimbwe kwa kutenganisha udongo wa juu na wa chini.

Vipimo vya shimo ni vyema vikazingatiwa. Iwapo utachimba shimo la mviringo litafaa liwe na kipenyo cha sentimeta 60 hadi 90 na kina cha sentimeta 60 hadi 90.

Iwapo utachimba shimo la mstatili au mraba litakuwa na urefu, upana na kina cha sentimeta 60 hadi 90, kutegemea kiasi cha mbolea kilichopo na kiasi cha mvua kinachonyesha sehemu husika.

Uwekaji wa mbolea hufuatia mara tu baada ya mashimo kuwa tayari. Kiasi cha madebe 5 ya mbolea ya samadi iliyooza vizuri au mboji iwekwe kwenye lundo la udongo wa juu kando ya kila shimo na ichanganywe kisha mchanganyiko wa mbolea na udongo urudishiwe katika shimo kisha kijiti kichomekwe katikati ya shimo hilo, ilikuonyesha sehemu ambapo mche au chipukizi litapandwa.

Nafasi ya kupandia migomba

Mashimo yachimbwe kwa nafasi inayokusudiwa kutumika kati ya mashina ya migomba na kati ya mistari kama ifuatavyo:-

  • Migomba inaweza kupandwa kwa nafasi ya umbali wa mita 2.75 kwa 2.75 kwa migomba mifupi kama Kimalindi na Kisukari. (Mashina 1,331 kwa hekta).
  • Umbali wa mita 3 kwa mita 3 kwa migomba ya urefu wa kati kama Jamaica na Mshare (Mashina 1,110 kwa hekta).
  • Umbali wa mita 3.6 kwa mita 3.6 kwa migomba mirefu kama Uganda green (Mashina 760 kwa hekta).

Jinsi ya kupanda migomba

Wakati unaofaa kupanda (machipukizi ya) migomba ni mwanzoni mwa msimu wa mvua. Chomoa kile kijiti ulichoweka wakati wa kuchimba mashimo na chimba shimo la kiasi cha sentimita 30 x 30 katikati ya shimo lililojazwa mchanganyiko wa udongo na samadi kisha panda chipukizi hilo.

Rudishia udongo na hakikisha tunguu (sehemu ya mizizi ya mgomba) lote limefunikwa vizuri. Shindilia udongo ili chipukizi lisimame wima imara.

Machipukizi yanayotarajiwa kupandwa yanatakiwa kuondolewa mizizi yote ili kudhibiti minyoofundo na fukuzi wa migomba. Pia maji ya moto au dawa kama vile furadani inaweza kutumika.

Jinsi ya kupanda migomba
Jinsi ya kupanda migomba

Namna ya Kutunza Migomba

Uwekaji wa matandazwa (mulching)

Kazi hii ni vyema ikafanywa mara baada ya kupanda kama inawezekana. Matandazo yawe ni makavu na unene wa sentimeta 15 ili kuhifadhi unyevu, kuzuia magugu na yakioza yataongeza mbolea.

Uongezaji wa mbolea

Baada kupanda ni vyema kuongeza mbolea (samadi) madebe 2 kuzunguuka shina la migomba kila baada ya miaka miwili au mitatu. Mbolea hii inatakiwa kuchanganywa na udongo na kufunikwa kwa matandazwa.

Umwagiliaji maji shambani

Migomba huhitaji maji mengi. Wakati wa kiangazi Inafaa kumwagilia ili kuto kupunguza sana ukubwa na wingi wa ndizi zinazotarajiwa kuvunwa kwa mwaka. Kiasi cha maji kinachotakiwa kwa wiki ni milimita 25, yaani eneo linalo zunguka shina la migomba lilowe kabisa.

Kupunguzia machipukizi Inatakiwa kupunguza mimea ya migomba kwa kila shina na kubaki mimea mitatu tu, yaani Mgomba wenye ndizi (Mama), Mgomba mkubwa ambao bado haujazaa lakini unakaribia kuchanua (Mtoto), Mgomba mchanga uliochipua hivi karibuni (Mjukuu).

Shamba la migomba linalotunzwa vizuri
Shamba la migomba linalotunzwa vizuri

Uondoaji wa Majani Makavu

Mimea ya migomba inafaa iondolewe majani yote makavu ili kuondoa uwezekano wa kuwepo mazalia ya wadudu na magonjwa, kuruhusu mionzi ya jua na kufanya urahisi wa kuhudumia shamba. Pia hufanya shamba kuonekana safi.

Uondoaji wa ncha mwishoni mwa matunda

Baada ya mkungu kutoa ndizi, ua hunyauka na kubakiza ncha mwishoni mwa matunda. Ncha hizo hupaswa kuondolewa. Huduma hii husaidia kupunguza uwezekano wa kujeruhi matunda wakati wa kusafirisha jambo ambalo kupunguza ubora wa tunda.

Kuweka Miega

Miega ni nguzo au kamba ambazo hutumika kuzuia migomba iliyobeba mikungu mikubwa isianguke kutokana na uzito mkubwa. Miega ni ya lazima katika sehemu zenye upepo mkali. Kazi hii inatakiwa kufanywa kwa uangalifu ili isijeruhi ndizi na mgomba wenyewe.

Uondoaji wa kichombezo cha ua la kiume (Shumba) Uondoaji wa shumba huwezesha matunda kukua vizuri, kuongezeka uzito wa mkungu pia huzuia magonjwa kama vile ugonjwa wa mnyauko wa migomba (Banana Baterial Wilt), ugonjwa wa Majivu nchani mwa matunda (Cigar end rot). Ukataji hufanyika juu ya kovu la pili baada ya kichana cha mwisho, kwa kutumia kisu kikali.

Wadudu Hatari Wa Migomba

Vikongomwa wa Migomba (Cosmopolites Sordidus)

Vikongomwa wa migomba
Vikongomwa wa migomba

Vikongomwa ni wadudu hatari sana wa migomba duniani kote. Idadi ya vikongomwa inaweza kupunguzwa kwa kutumia vipanzi safi, kuharibu mabaki ya mimea na kutumia mwarobaini. Hata hivyo, kuhamia kwa vikongomwa kutoka kwa mashamba jirani kunaweza kupunguza ufanisi wa njia zozote za kukabiliana nao.

Vikongomwa wa ndizi (Cosmopolites sordidus) pia wanajulikana kama banana borer au banana root borer. Vikongomwa huenea kati ya mashamba, wilaya na nchi kwa usafirishaji wa sehemu za migomba zilizoathirika, hasa viazi (moyo wa mgomba).

Vikongomwa vilivyokomaa vinaweza kutembea kwa urahisi kutoka kwa mgomba mmoja hadi mwingine.

Dalili muhimu

  • Vikongomwa ni wadudu wakubwa ambao hushambulia aina zote za migomba (Musa spp.) na ensete (Ensete spp.).
  • Dalili ni pamoja na mahandaki, miche dhaifu au inayokauka, majani ya rangi ya manjano yanayoning’inia na mikungu midogo ya ndizi. Mimea iliyoathirika sana huonyesha uharibifu mkubwa kwa shina na mashambulizi makali yanaweza kusababisha mgomba kuanguka.
  • Viazi vilivyoathirika vitakuwa na matundu ya upana wa hadi sentimita 1.5. Ili kutambua wadudu, kata kiazi chenye matundu na mahandaki ili kubaini kama mabuu yako ndani.
  • Migomba iliyo dumaa na ile inayoonyesha kunyauka mapema kwa majani pia inapaswa kukaguliwa kama ina mabuu na vikongomwa vilivyokomaa. Ipasue kwa kutumia kisu au kata  shina juu kidogo ya usawa wa ardhi  ili kutafuta mabuu au mahandaki yao.
  • Vikongomwa waliokomaa huvutiwa zaidi na viazi na mashina yaliyokatwa ambayo yanaweza kutumika kama mitego kwa ajili ya ufuatiliaji.

Ueneaji wa vikongomwa

Vikongomwa vya ndizi vilitokea nchini Malaysia na Indonesia, na kwa sasa vinapatikana katika maeneo yote makuu yanayozalisha ndizi duniani. Vinapatikana Afrika Mashariki na Magharibi ikiwa ni pamoja na Burkina Faso, Ghana, Mali, Nigeria, Tanzania, Uganda na Kenya.

Athari za vikongomwa

  • Vikongomwa wa ndizi hupunguza ukuaji wa mizizi, hupunguza uwezo wa kuchukua virutubishi na nguvu ya mmea, na husababisha kuzaliwa kwa mikungu midogo ya ndizi na mazao kidogo na kudhoofisha afya ya mimea.
  • Mashambulizi katika shamba jipya lililopandwa husababisha mmea kushindwa kukua. Ndizi za nyanda za juu na plantain huathirika zaidi kuliko za kuivishwa  au za kutengeza pombe.

Jinsi ya kujikinga na vikongomwa

  • Kuweka vizuizi vya karantini katika kila eneo na kuhakikisha uwepo na utumizi wa mbegu safi za kupanda ni njia muhimu za kukinga mimea mipya dhidi ya mashambulizi na kuzuia kuenea kwa wadudu.
  • Ni muhimu sana kwa wakulima kutumia vipanzi safi. Wakulima wanatakiwa kukagua viazi na miche ili kubaini uharibifu na kuondoa yote ambayo imeathirika. Chukua kipande kimoja au viwili kutoka kwa vipanzi na uangalie kama kuna mahandaki, mabuu au pupae. Kama vimeathirika, haribu hiyo mbegu.
  • Kama vipanzi safi havipatikani, basi kukata mbegu ili kuondoa sehemu zilizoathiriwa na mayai na mabuu, na kutumia maji ya moto kutibu vipanzi ni njia mbili bora. Bambua ganda la nje la mche ili kuondoa mayai ya vikongomwa. Tumbukiza mche safi ndani ya maji ya moto (joto la kiwango cha nyuzi 52 hadi 55) kwa dakika 15 hadi 27 kabla ya kupanda.
  • Mwarobaini pia unaweza kutumika kwa ufanisi kusafisha vipanzi. Tumbukiza machipukizi kwa mafuta ya tembe za mwarobaini kiwango cha asilimia 20 kabla ya kupanda.
  • Kuvu wa kuua wadudu, kama vile Beauveria bassiana na Metarhizium anisopliae, na wadudu wengine wa kuthibiti kibiolojia (mfano athropoda kama vile mchwa) wanafanyiwa majaribio na kuendelezwa na wanaweza kutoa suluhisho zaidi katika siku zijazo.

Jinsi ya kuthibiti vikongomwa

Haribu mabaki yote ya mimea iliyoathiriwa baada ya kuvuna ili kupunguza idadi yao.

Usirudie kupanda kwenye maeneo yalioathirika kama viazi vya mgomba bado viko kwa ardhi. Ondoa viazi vyote baada ya mavuno ya mwisho, vikatekate vipande 4 hadi 8 na uviwache vikauke ili kuzuia mabuu yasiendelee kuishi katika migomba iliyovunwa ndizi. Ngojea kwa muda wa miezi 3 ili vikongomwa wafe, kabla ya kupanda tena katika hilo shamba.

Magonjwa ya Migomba

Mnyauko Bakteria wa Migomba (Xanthomonas Campestris Pv. Musacearum)

Ugonjwa wa mnyauko bakteria wa migomba
Ugonjwa wa mnyauko bakteria wa migomba

Ugonjwa wa Banana Xanthomonas wilt (BXW) umepewa jina lake kutoka kwa bakteria wanaoambukiza na hatimaye kuua mgomba. Ugonjwa huo umeongezeka sana Uganda tangu ulipopatikana kwa mara ya kwanza mwaka wa 2001 na sasa umeenea katika kanda yote.

Aina zote za migomba hushambuliwa ingawa matokeo ya utafiti yameonyesha uwezekano wa kupatikana kwa aina sugu siku zijazo. Aina kuu ya usimamiaji kwa sasa ni kuzingatia usafi wa shamba: kupanda mazao ya afya, kutumia zana safi za kukatia na kuondoa maua dume ili kupunguza kuathiriwa kupitia wadudu wanaobeba bakteria wakati wanapofyonza utomvu.

Ugonjwa wa BXW haupatikani Afrika Magharibi; na ule ugonjwa mwengine mkubwa zaidi wa mnyauko bacteria duniani kote unaosababishwa na Ralstonia solanacearum (ugonjwa wa Moko), haupatikani kote Afrika.

Visababishi vya Mnyauko bakteria wa migomba

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria Xanthomonas campestris pv. musacearum. ‘pv.’ inasimama kwa neno ‘pathovar’ na inaonyesha aina fulani ya X. campestris ambayo huambukiza tu migomba pekee na jamii yake ya karibu ya ensete. Hapo awali ilikuwa inajulikana kama X. musacearum.

Dalili muhimu za Mnyauko bakteria wa migomba

  • Alama kubwa zaidi ya ugonjwa wa BXW ni kuwa ndizi huiva mapema kabla ya kukomaa: Vidole kadhaa huanza kuwa na rangi ya manjano na vyengine kwenye mkungu kubakia rangi ya kijani. Vikikatwa, vidole huwa na rangi nyeusi hata pamoja na vile ambavyo ni rangi ya kijani. Vidole huwa vyeusi kwa haraka na hatimaye mkungu wote huoza.
  • Ishara ya kwanza ya maambukizi, hata hivyo, ni wakati majani ya rangi ya zambarau ya maua ya kiume hunyauka, kuwa meusi na kufa. Pia angalia majani machanga sehemu ya juu ambayo hugeuka rangi ya manjano, kukunjika katikati na kisha kuanguka.
  • Kata shina la mkungu, na utomvu unapoisha kutoka angalia madoa madogo ya rangi ya manjano. Haya yanaonyesha kwamba bakteria wanazuia mtiririko wa maji na virutubishi. Hata hivyo, inawezekana kuwa vigumu kuona madoa haya madogo ya rangi ya manjano.
  • Ugonjwa wa kuvu wa migomba, unaojulikana kama Fusarium wilt au ugonjwa wa Panama, pia husababisha rangi ya manjano lakini kwenye majani yaliyozeeka. Jani halijikunji na manjano yake ni kali zaidi ikilinganishwa na BXW.
  • Matunda huendelea kawaida. Dalili ya kutofautisha Fusarium wilt ni rangi nyeusi ndani ya shina, ambayo haiko kwenye migomba iliyoambukizwa na mnyauko bakteria.                      

Athari za mnyauko bakteria wa migomba

Ugonjwa wa mnyauko wa migomba ni ugonjwa hatari sana, umeua migomba mingi sana mkoani kagera tangu ulipoingia kwa mara ya kwanza. Huu ugonjwa ndio uliwafanya ndugu zetu Wahaya waache kutegemea ndizi kama zao lao kuu, na hivyo kuanza kulima mazao mengine ya chakula.

BXW ni ugonjwa mharibifu sana unaoathiri kila aina ya migomba. Mimea na matunda huharibiwa. Ugonjwa unaweza kuenezwa mbali kwa njia ya vipandikizi na mabaki ya mimea. Haja kubwa ya ndizi katika Kampala huvutia kuletwa kwa bidhaa kutoka mbali.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Mnyauko bakteria wa migomba

Mbinu za kitamaduni

  • Ugonjwa wa BXW huenea kwa njia ya machipukizi ya kupanda, na wadudu ambao huingiza bakteria kupitia maua ya mgomba. Bakteria pia wanaweza kusafirishwa kwenye zana za kukatia.
  • Aina zote za migomba hushambuliwa ingawa ni vigumu kwa bakteria kuambukiza baadhi ya aina mashambani kwa sababu ya hali zao za maua. Aina hizi pia zinaweza kuambukizwa kwa kupitia zana za kukatia ambazo zimebeba bakteria.
  • Njia muhimu kwa mafanikio ya udhibiti ni uchaguzi makini wa machipukizi yasiyokuwa na ugonjwa na kuweka zana za kutumika kwa ajili ya kukata mikungu ya ndizi na majani kuwa safi na zisizo na bakteria.
  • Chagua kwa makini machipukizi ya kupanda kutoka maeneo ambapo ugonjwa huo hauko. Pata machipukizi kutoka kwa vyanzo vya kuaminika. Usitumie machipukizi kutoka kwa mimea iliyoathiriwa na BXW, hata kama machipukizi yataonekana kuwa yenye afya.
  • Kuondolewa kwa ua dume kwa kutumia mkono au mti panda (ili kupunguza hatari ya kuhamisha bakteria kupitia zana za kukata) kutapunguza athari ya kuambukizwa kupitia wadudu wanaobeba mbelewele na utomvu ambao awali wamezichukua kutoka kwa mimea iliyoambukizwa.
  • Majira ya kuyaondoa ni muhimu; maua dume yanastahili kukatwa haraka baada ya chana ya mwisho. Shida ya njia hii ni kwamba huchukua muda mwingi na baadhi ya wakulima wanaamini kuwa ua dume ni muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa juisi nzuri katika aina ya ndizi za kutengeza bia.

Mbinu za kikemikali

Vifaa vya kukata vinaweza kusafishwa kwa kutumia dawa ya jik (sehemu moja ya dawa na sehemu nne za maji), dawa za mimea ya kienyeji zenye uwezo wa kuua bacteria, kama vile tumbaku au pilipili, au kwa kupitisha kwenye moto. Jik ni njia ya ufanisi zaidi kwa kuua bakteria ingawa wakulima wachache huonekana kutumia njia hii.

Jinsi ya kutibu ugonjwa wa Mnyauko bakteria wa migomba

Mbinu za kitamaduni

Ushauri wa awali wakati BXW ilipogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Uganda ulikuwa ni kuchimba na kuchoma koo zima la mgomba. Sasa tunajua kwamba bakteria hawavamii kabisa mmea wote. Ushauri sasa hivi kwa hivyo, ni kung’oa mashina yanayoonyesha dalili ya BXW na kuyatupa kwa makini.

Kutoa shina moja kutapunguza kiasi cha bakteria wanaoweza kuambukiza mimea mipya, lakini hii haitaondoa kabisa ugonjwa. Kuchagua vipandikizi vyenye afya na kusafisha vifaa vya kufanyia kazi ndio ushauri mhimu wa kufuata uliobaki.

Mbinu za kikemikali

Mmea unapoambukizwa, hakuna tiba ya kudhibiti ugonjwa huo.

Mnyauko Fusari Wa Migomba (Fusarium Oxysporum F.Sp. Cubense)

Ugonjwa wa mnyauko fusari wa migomba
Ugonjwa wa mnyauko fusari wa migomba

Mnyauko wa fusarium, pia unaojulikana kama ugonjwa wa Panama, ni ugonjwa mbaya sana unaoathiri migomba. Unasababishwa na kuvu linaloishi mchangani Fusarium oxysporum f.sp. cubense.

Mnyauko wa fusarium wa migomba na plantain ni kuvu ambalo huathiri mizizi na shina la migomba, huziba njia za kupitisha maji na kusababisha majani kugeuka rangi ya manjano, kukauka na mwishowe kuanguka.

Husambazwa kwa njia ya kuhamisha udongo, kwa vifaa vya shambani na hasa kwa chipukizi zinazotumika kwa kupanda.

Kuna aina nne tofauti za fusarium wilt, tatu zinaweza kuzuiwa kwa mbinu za kitamaduni na kwa kutumia aina sugu, lakini aina ile ya nne iliyogunduliwa hivi karibuni (TR4) inashambulia ndizi za aina zote mbili, hii inaleta athari kubwa kwa viwanda na kwa uzalishaji mdogo wa ndizi.

Hivi karibuni, kuvu limesambaa kutoka Asia ya Kusini na Australia, Jordan na Msumbiji.

Dalili muhimu za mnyauko fusari wa migomba

  • Dalili ya kwanza ni rangi ya manjano pembezoni mwa majani yaliyozeeka, ikielekea katikati mwa jani. Majani hugeuka rangi ya kahawia, hukauka na hatimaye huanguka.
  • Dalili za ugonjwa huendelea kutoka kwa majani yaliyozeeka na kupanda juu, hatimaye majani machache machanga yaliyo wima na yenye rangi ya kijani kibichi hubakia; majani yaliyozeeka hulifunika shina mfano wa kirinda (skirt), mwishowe majani yote huanguka. Kwa aina nyingine za ndizi shina pia hupasuka.
  • Miviringo ya rangi za kahawia, nyekundu na manjano hufanyika kwa ndani, kwanza katikati, kisha baadaye kama maambukizi ni makali sana, huenea hadi shina lote. Miche pia yaweza kuonyesha dalili hizo. Hatimaye sehemu zote zilizo juu na chini ya ardhi zitakufa na kuoza.
  • Athari za mnyauko fusari wa migomba
  • Jamii ya kwanza ililazimisha sekta ya mauzo ya nje ya ndizi kubadilisha kutoka aina ya Gros Michel na kuanza kuuza Cavendish katika miaka ya 1950, wakati mnyauko wa fusarium ulipomaliza kabisa mazao. Jamii nyingine zimejitokeza tangu wakati huo.
  • Mbali na kuharibu mazao, pia itatatiza maisha na usalama wa chakula wa mamilioni ya wakulima wadogo ambao wanakuza zaidi ya aslimia 85 ya zao hilo.
  • Zaidi ya hayo, kuna uwezekano wa athari za kimazingira na utofauti wa viumbe hai kwa kuwa mashamba ambayo hayajaathiriwa yatatayarishwa kwa ajili ya kilimo na aina za mbegu zenye matatizo zitawachwa.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa mnyauko fusari wa migomba

Ni vigumu sana kujikinga na ugonjwa wa mnyauko fusari kwa sababu kuvu huishi kwa udongo kwa miaka mingi na hakuna dawa za kuvu ama mbinu mwafaka za kitamaduni zinazoweza kulidhibiti kuvu kikamilifu.

Suluhisho zilizoko ni:

  • Epukana nalo ikiwezekana;
  • Buni mbinu za kuutambua ugonjwa mapema;
  • Dumisha usafi; na
  • Tumia aina sugu.

Jinsi ya kutibu ugonjwa wa mnyauko fusari wa migomba

Ikiwa mgomba ulioathirika umetambuliwa, jaribu sana usiusumbue udongo ulio karibu nao. Chimba mgomba huo na mizizi yake yote pamoja na miche yote na kuichoma hapo hapo. Usiukatekate vipande. Tumia dawa ya kuua kwekwe (kwa mfano glyphosate) ili kuharakisha kufa kwa mmea ulioathirika halafu uuache ufe hapo hapo.

Sigatoka Nyeusi Ya Migomba (Mycosphaerella Fijiensis)

Ugonjwa wa sigatoka nyeusi ya migomba
Ugonjwa wa sigatoka nyeusi ya migomba

Sigatoka nyeusi inayosababishwa na kuvu Mycosphaerella fijiensis, ni ugonjwa wa majani ya migomba ulimwenguni. Mbegu zake husambazwa kupitia upepo na mvua, majani hufa haraka baada ya maambukizi, hupunguza uzani wa ndizi kwa kiwango cha asilimia 30 hadi 40 – na kwa kiwango kidogo zaidi kwa ndizi aina ya plantain.

Usimamizi wake ni kwa kutumia aina za migomba zinazovumilia au za sugu. Migomba aina ya plantain hushambuliwa kwa kiwango kidogo na aina sugu za ndizi za kuivisha na/au za kupika zenye sifa ya Cavendish zimezalishwa.

Dalili muhimu wa sigatoka

  • Dalili ya kwanza ya ugonjwa huu ni mistari ya rangi nyekundu-kahawia inayoenda sambamba na mishipa ya jani, yenye urefu wa milimita 1 – 5 na upana wa milimita 0.25. Huwa inaonekana sana upande wa chini wa jani changa la tatu au la nne, hususan katika ukingo wa jani unaojitokeza kwanza jani likichomoza.
  • Mistari hupanuka na kuonekana upande wa juu wa jani, ikigeuka myeusi halafu baadaye hubadilika kuwa kijivu, katikati iliyobonyea kidogo na kingo nyeusi na kanda za rangi ya manjano. Mistari inapoungana hutengeza mikusanyiko ya maeneo ya kufa yenye upana wa sentimita kadhaa kila upande wa katikati ya jani, na majani huvunjika na kufa.

Athari za ugonjwa wa sigatoka

  • Sigatoka nyeusi ni ugonjwa mbaya zaidi wa majani ya migomba na umeenea sehemu zote za tropiki. Majani hufa mapema, huishi siku 50 badala ya siku 200 kama ilivyo kawaida. Matokeo yake ni kuwa na majani chini ya 5 hadi 7 wakati wa kutoa maua, ambacho ndicho kiwango cha chini kabisa cha majani kinachotakiwa ili kupata mkungu wa ndizi wenye uzani na ubora unaokubalika.
  • Athari ya sigatoka nyeusi inaweza kupimwa kwa njia tofauti, kutegemea kama ndizi zimepandwa kwa ajili ya biashara au matumizi ya nyumbani, na pia kama ndizi za kawaida au plantain ndilo zao la muhimu.
  • Makadirio yatatofautiana katika sehemu mbalimbali za dunia, lakini kwa ujumla hasara katika ndizi za Cavendish inayosababishwa na sigatoka nyeusi ni asilimia 30 hadi 40 ambayo ni upungufu wa mazao, kutokomaa ama ndizi kutoiva kwa pamoja. 
  • Ili kuepuka hasara kubwa, madawa ya kuzuia kuvu hutumiwa. Madawa haya huwa asilimia 30 ya gharama ya uzalishaji.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa sigatoka

  • Udhibiti wa ugonjwa huu ni mgumu sana na njia bora ni kwa kutumia aina za mbegu ambazo zinaweza kustahimili au ni sugu, na kuzingatia mbinu za kitamaduni ambazo zitapunguza muda wa majani kukaa na  unyevu na kusababisha kushambuliwa.
  • Kwa upandaji mzuri chagua sehemu za mchanga unaopitisha maji na hewa vizuri, na uepuke sehemu zenye udongo mzito wa ngama ambao husimamisha maji kwa muda baada ya mvua. Epuka mahali kwenye kivuli cha miti.
  • Ikiwa unapanda katika sehemu za milima, chagua sehemu ambako jua la asubuhi huangaza ili kukausha umande ulioko kwenye majani kwa haraka.
  • Daima panda kwa miraba ikielekea upande upepo unavyoenda ili kuruhusu hewa kuingia na kukausha maji kwenye majani, ili kuzuia maambukizi na kupunguza idadi ya mbegu za kuvu. Kupanda kwa hatua pana kama mita 2.5 (migomba 1600 kwa hekta) pia kutasaidia.
  • Tumia aina za mbegu zinazohimili au za sugu. Aina nyingi za migomba ya plantain huhimili au ni sugu (kwa mfano Mysore, Saba na Pisang Awak). Kuna aina za kuivisha na za kuivisha/kupika ambazo ni sugu kwa sigatoka nyeusi. Yangambi Km5, ndizi ya kuivisha kutoka Afrika Magharibi pia ni sugu kwa sigatoka nyeusi. Angalia kama aina hizi za migomba zinapatikana katika eneo lako.

Jinsi ya kutibu ugonjwa wa sigatoka

Mbinu za kitamaduni

Kusanya majani yalioathiriwa, yaliyobaki kwa mgomba baada ya kuvuna ndizi, uyatoe nje ya shamba na uyachome.

Mbinu za kikemikali

  • Kukata majani na kutumia madawa ya kuzuia kuvu ni muhimu kama migomba aina ya Cavendish imepandwa kwa ajili ya biashara. Kukata majani yalioathiriwa hufanywa kabla ya kunyunyiza dawa.
  • Ondoa majani au sehemu za majani zilizoathiriwa. Kama athari ni chini ya asilimia 30, kata sehemu ya jani iliyoathiriwa, kama ni zaidi ya asilimia 40 toa jani lote. Peleka majani uliyokata nje ya shamba na uyachome.
  • Dawa za kuzuia kuvu zinazobakia juu ya jani: Mancozeb (iliyo changanywa na mafuta au maji na mafuta) na chlorothalonil (iliyochanganywa na maji) hutumika wakati ugonjwa uko kwa kiwango cha chini.
  • Dawa zinazozuia kuvu zinazoingia ndani ya mmea: Triazoles (Kwa mfano, propiconazole, fenbuconazole na tebunconazole) na strobilurins (kwa mfano, azoxystrobin).
  • Ni muhimu kubadilisha dawa za kuzuia kuvu za makundi mbalimbali ili kuzuia kuongezeka kwa usugu wa aina za kuvu dhidi ya hizo dawa. Usitumie zaidi ya mara mbili aina moja ya dawa zinazoingia ndani ya mmea bila ya kubadilisha kundi lingine. Wakati wa ukame, mancozeb inaweza kutumika peke yake.

Bunchy Top Ya Migomba (Banana Bunchy Top Virus)

Bunchy top ya migomba ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoingia ndani ya mmea na kukaa humo. Vipanzi vilivyoambukizwa huonekana kuwa na afya. Vidukari wanaopatikana katika nchi zote zinazokuza migomba husaidia kusambaza ugonjwa maeneo ya karibu.

Mashada ya majani yaliyosimama yanayosababishwa na ugonjwa huleta udadisi zaidi. Mmea hautoi matunda na uzalishaji wa ndizi huathirika sana. Migomba yote yaweza kushambuliwa na hakuna tiba ya kikemikali.

Hata hivyo, uchaguzi makini wa vipanzi vyenye afya, unaweza kuzuia kuanzishwa kwa ugonjwa kwa nchi mpya na kutambua mapema dalili kutawezesha kupunguza kuenea kwake.

Dalili muhimu za bunchy top

  • Maendeleo au kuonekana kwa dalili kunategemea jinsi mmea utakavyoambukizwa. Majani ya kwanza (machipukizi) kutoka kwa shina lililoambukizwa au mmea mama (maambukizo ya msingi) ni madogo na yamekusanyika pamoja.
  • Hukaa wima na hayajipindi nje kama majani ya mgomba wenye afya. Pembezoni mwa jani huwa rangi nyepesi (chlorotic), ikienda kuwa kahawia kuelekea katikati yake.
  • Majani mapya kwa mfululizo huwa membamba na madogo, na kuonekana wazi kuwa kama shada. Chipukizi kutoka shina lote lililoambukizwa ni nadra kutoa matunda.
  • Maambukizi ya pili hutokea wakati vidukari wanapoingiza virusi kwa mmea wenye afya. Mara ya kwanza maendeleo ya dalili huwa si makubwa na ni vigumu zaidi kuziona ikilinganishwa na vichipukizi vilivyoambukizwa.
  • Jani la pili linalozaliwa baada ya virusi kuingia hutoa vistari vifupi vya kijani kibichi kwenye mishipa yake midogo ambavyo huonekana kama dash, ingawa hivi huwa vigumu kuvitofautisha.
  • Mishipa huwa kama ndoano (umbo la herufi -J) inapoungana na uti wa katikati ya jani. Maumbo ya ‘J’ na vistari vidogo huonekana vizuri chini ya jani ukiliangalia dhidi ya mwangaza. Alama za dash pia zinaweza kuonekana kwenye uti wa jani na kwenye shina kuu la mgomba.
  • Dalili za awali za maambukizi ya pili zaweza kufikiriwa kimakosa kuwa ni upungufu wa madini au dhiki ya kimwili wala sio ya kibiolojia. Bunchy top inadhihirika wakati kila majani yanayozaliwa baadaye kwa mfululizo yanakuwa madogo zaidi.
  • Muundo wa shada hauonyeshi sana, ingawa bado unaweza kuonekana, kama maambukizi ya pili yanafanyika katika hatua ya baadaye ya maendeleo ya mgomba.
  • Mgomba wenye maambukizi ya pili unaweza kutoa ndizi mara moja lakini zitakuwa ndogo na zenye umbo lisilo la kawaida. Vichipukizi vipya vitakuwa na virusi na vitazaa majani ambayo yameathirika kutoka mwanzo.

Athari za ugonjwa wa bunchy top

Bunchy top ni moja ya magonjwa makubwa zaidi ya migomba. Katika mimea iliyoambukizwa sana, hasara ya mavuno yote inaweza kutokea. Ugonjwa uliozuka Malawi katika miaka ya kati ya 1990 uliathiri hekta 3500 na unakadiriwa kuwa uliharibu hekta 800.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa bunchy top

  • Virusi hutembea ndani ya mmea wote na vinaweza kuwa katika sehemu zisizoonyesha dalili, hivyo umuhimu wa kuhakikisha kuwa nyenzo zinazotumika kwa ajili ya uenezi, kama vile viazi na vichipukizi, havina virusi.
  • Ni muhimu kuchunguza nyenzo zinazotumika kwa tissue culture ili miche iwe haina virusi.
  • Nyenzo za kupandia zenye afya lazima ziwepo ili wakulima waweze kuzipata.
  • Hakuna udhibiti wa kibiolojia kwa vidukari wa migomba.

Jinsi ya kutibu ugonjwa wa bunchy top

Mbinu za kitamaduni

  • Uangalizi wa mara kwa mara (kwa mfano kupitia kliniki za mimea) na tafiti za mara kwa mara zinazofanywa na watumishi wa nyanjani ni muhimu ili kuhakikisha kuwa milipuko yoyote inaonekana mapema na kushughulikiwa haraka.
  • Ikionekana, migomba iliyoathirika yapaswa kung’olewa na kukatwa vipande vidogo vidogo ili kuzuia vichipukizi vipya kumea.

Mbinu za Kikemikali

  • Hakuna udhibiti wa kemikali kwa virusi hivi, aidha kama hatua ya kukinga au kutibu. Kemikali zinaweza, hata hivyo, kutumika dhidi ya vidukari ambao hueneza ugonjwa.
  • Mimea iliyoambukizwa yaweza kunyunyiziwa, hasa upande wa chini wa majani, kwa nguvu na maji au ufumbuzi wa maji na sabuni (kama asilimia 2 kwa kipimo) kuua vidukari na hivyo kusaidia kuzuka kwa mapema.
  • Mafuta yenye dawa za kuua wadudu pia yanaweza kutumika, kama vile yale yenye mafuta ya taa au maji ya dawa yanayotokana na majani ya mwarobaini (dondoo asilimia 2 kwa kipimo).

Uvunaji wa Ndizi

Muda wa uzalishaji ndizi

Zao la ndizi huchukua miezi 9 hadi miezi 15 tangu kupandwa kwa chipukizi mpaka kuanza kuvunwa. Muda wa kuvuna hutegemea hali ya hewa. Katika sehemu za joto ndizi huvunwa mapema zaidi kuliko sehemu za baridi.

Pia migomba iliyopandwa kwa kutumia machipukizi huzaa mapema zaidi kuliko iliyopandwa kwa miche iliyozalishwa kwa chupa (tissue culture).

Mkungu wa ndizi kwenye mgomba
Mkungu wa ndizi kwenye mgomba

Matumizi ya riboni

Riboni za rangi moja (au alama ya kamba) hufungwa kwenye migomba ya umri mmoja mara tu inapoanza kuchanua, na riboni ya rangi nyingine hufungwa kwenye migomba itakayoanza kuchanua wiki mbili hivi zinazofuata na kuendelea hivyo ili kurahisisha kuitambulisha mikungu ambayo itavunwa kwa wakati mmoja.

Pia matumizi ya riboni hurahisiha utunzaji wa kumbukumbu ili kujua ni lini na ni mikungu mingai itavunwa.

Mavuno ya ndizi kwa ekari

Mavuno ya ndizi hutegemea zaidi aina ya migomba, hali ya hewa, na utunzaji wa migomba shambani. Mavuno huweza kufikia hadi tani 25 au zaidi kwa ekari kwa mwaka. Hata hivyo mavuno mazuri kwa mkulima wa kawaida yasipungue kati ya tani 8 na 12 za ndizi kwa ekari kwa mwaka.

Wakati unaofaa kuvuna

  • Mkungu wa ndizi huvunwa katika hatua tofauti kulingana na matumizi, aina na mahitaji ya soko.
  • Mkungu huachwa kwenye mgomba mpaka vidole (matunda) vimejaa. Uzito wa mkungu hongezeka haraka katika wiki mbili za mwisho, ambapo migongo ya ndizi hutoweka.
  • Ndizi zinaweza kuvunwa zikiwa zimekomaa na zimeiva kwa kiasi cha asilimia 75 kwa ajili ya kusafirishwa mbali, pia zinaweza kuvunwa zikiwa zimekomaa na zimeanza kuiva kwa ajili ya soko la karibu, au zikiwa zimekomaa na kuiva kabisa kwa ajili ya soko na matumizi ya nyumbani.
  • Njia bora ya kukata mkungu, ni ile inayohakikisha kuwa mkungu wa ndizi hauanguki chini na kuvunja, kuchubua au kuharibu ndizi, jambo ambalo litapunguza ubora. Ukichelewa kuvuna ndizi zinaweza kuharibiwa na ndege, wanyama, wadudu au kuibiwa.

Ubora wa ndizi

Ndizi zenye sifa nzuri sokoni ni zile ambazo zimekomaa kwa kiasi kinachotakiwa na zenye vidole vyenye urefu mzuri na visivyo na michubuko. Pia ziwe hazijashambuliwa na magonjwa wala wadudu waharibifu

WhatsApp/call 0683308173

Email shafii.ismail09@gmail.com


http://www.kilimoniuhaiblog.blogspot.com

0 comments: